Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Vituo vya Redio Jamii hapa Nchini vinapaswa kuwa chem Chem ya elimu itakayotoa manufaa kwa Jamii inayovizunguuka Vituo hivyo badala ya utaratibu wa kurusha vipindi vya muziki wakati wote.

Kauli hiyo aliitoa wakati akiizindua Redio Jamii ya Wilaya ndogo ya Tumbatu hapo katika jengo la Wilaya hiyo liliopo katika Kijiji cha Kichangani ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Balozi Seif alisema mijadala na nakala zinazohusiana na mausla ya Uchumi, siasa, jamii na Maendeleo ndio lengo lililokusudiwa katika uanzishwaji wa Redio hizo na kupelekea kuungwa mkono na Taasisi na mashirika ya maendeleo Duniani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka watendaji wa Redio Jamii Tumbatu kujitahidi kuwaelimisha wananchi kuhusu uvuvi bora na mambo mengi yanayohusiana na bahari kwani maisha ya wananchi hao yametegemea zaidi sekta ya bahari. 

“ Tunategemea redio yenu ya jamii hapa Tumbatu itajikita zaidi katika kuwaelimisha wananchi wa Kisiwa hichi na maeneo ya jirani kuhusu athari za uvuvi haramu ambao unapigwa vita na Serikali kisheria “. Alisisitiza Balozi Seif.

Alitahadharisha jamii kwamba vyombo vya habari vina nguvu kubwa ambayo kama itatumika vibaya inaweza kuleta mifarakano mikubwa katika jamii na hivyo basi usalama na amani unaweza kuhatarishwa.

Balozi Seif alifahamisha kuwa chokochoko na fitna za kisiasa zikiachiwa na kuelekezwa katika vituo vya redio Jamii ni mwanzo wa kuathirika kwa vituo hivyo, watendaji pamoja na wananchi wenyewe.

“ Nia ya Redio jamii ni kuelimisha jamii na sio kupotosha. Hivyo Wanahabari wa Redio hizi wanapaswa kufanya utafiti wa kina wa Habari zao kabla ya kuzitoa, vyenginevyo zinaweza kupotosha jamii “. Alifafanua Balozi Seif.

Alileza kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona vyombo vya Habari na utangazaji nchini vinasaidia kudumisha na kuimarisha usalama na amani hatimae kupata maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka watendaji wa Redio hiyo redio nafasi kwa wananchi wa rika, jinsia na kila makundi yote yanayostahiki kusikika katika jamii inayowazunguuka.

Balozi Seif aliishukuru Jumuiya ya Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa {UNESCO } kwa msaada wake mkubwa wa vifaa vya studio na mitambo ya kurushia matangazo kwa Redio Jamii ya Tumbatu. 

Aliiomba taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa kuendelea kusaidia harakati nyengine za kijamii kila hali inaporuhusu na kitendo cha Uongozi wa Jumuiya hiyo kuahidi kukamilisha changamoto zinazokikabili kituo hicho ndani ya mwezi mmoja ujao ni cha kupigiwa mfano.

Akisoma Risala ya Wananchi wa Kisiwa hicho Afisa Tawala wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Redio hiyo Nd. Mohd Omar Hamad alisema uongozi wa Redio hiyo umekusudia kutoa vipindi vitakavyotumiwa na wanafunzi wa Maskuli na Madrasa za eneo hilo.

Nd. Mohd alisema utaratibu huo ambao ni miongoni mwa mpango kazi wa Redio hiyo utasaidia wanafunzi hao kujiimarisha zaidi kielimu kwa kujijengea uwezo mkubwa wakati wanapokabiliana na mitihani yao.

Hata hivyo Afisa Tawala huyo wa Wilaya ndogo ya Tumbatu alielezea changamoto zinazokikabili kituo hicho cha Redio jamii Tumbatu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa jengo la kudumu ambapo hivi sasa wanatumia jengo la Ofisi ya Wilaya hiyo.

Akitoa Salamu za Jumuiya ya Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa { UNESCO } Mwakilishi wa Jumuiya hiyo Nchini Bwana Abdullwahabi Koribaly alisema Taasisi yake itaendelea kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo katika kuunga mkono Vituo vya Redio Jamii.

Bwana Abdullwahabi alisema Redio Jamii Tumbatu iliyopata ufadhili wa Jumuiya hiyo ya Umoja wa Mataifa ya Unesco ina uwezo wa nguvu za Walti 300 ambazo zinaweza kuhudumia wasikilishaji zaidi ya Laki 150,000.

Akimkaribisha mgeni rasmi Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema Redio Jamii Nchini tayari zimeshaonyesha mafanikio makubwa kwa kuisaidia kubadilisha mazingira ya Jamii kupitia taaluma inayotolewa kwenye vipindi vya Vituo hivyo.

Waziri Mbarouk alifahamisha kwamba Zanzibar hivi sasa ina vituo ishirini vya matangazo ya redio ikilinganishwa na kituo kimoja tuu cha Redio cha Serikali { STZ } kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alieleza kwamba kadri hali ya maisha inavyobadilika ndivyo sekta ya Habari inavyopanuka ikitoa fursa pia kwa redio nyengine za Jamii zilizoanzishwa katika Wilaya ya Micheweni Pemba na Mtengani Makunduchi Kusini Unguja kwa msaada mkubwa wa UNESCO kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Redio Jamii ya Kisiwa cha Tumbatu inayotumia masafa ya 94.99 F.M inasikika katika umbali wa Kilomita zaidi ya 15 unaokizunguuka kituo hicho. Hata hivyo Redio hiyo pia inawqeza kusikika hata katika eneo la Mji wa Zanzibar kutegemea hali ya hewa iliyopo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiambatana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk, Naibu wake Mh. Bihindi Hamad na baadhi ya viongozi wa Serikali walifika Kijiji cha Uvivini Tumbatu kuzifariji familia za watu waliofariki dunia juzi kwa ajali ya gari.

Watu hao waliofariki Marehemu Ali Gora Haji na Marehamu Khamis Bakari Haji wakaazi wa Bububu wakiwa wazaliwa wa Tumbatu walipatwa na mauti hayo wakiwa safarini kuelekea Bumbuni kuhudhuria maulidi ya kuzaliwa kwa Mtyume Muhammad { SAW }.

Akitoa mkono wa pole kwa familia za marehemu hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwataka ndugu na jamaa wa marehemu hao kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha maombolezi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top