Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesifu maendeleo yaliyopatikana katika skuli ya msingi ya ALI KHAMIS CAMP inayosimamiwa na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ). 

Amesema skuli hiyo imekuwa na maendeleo ya kupigiwa mfano kwa skuli za Tanzania, na kwamba yamepatikana kutokana na umakini na nia njema ya jeshi hilo katika kuwapatia watoto elimu bora. 

Maalim Seif ametoa pongezi hizo katika skuli hiyo, wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi za elimu kisiwani Pemba. 

Aidha amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na mashirikiano makubwa yaliyopo kati ya wananchi, Wizara ya elimu pamoja na Jeshi hilo, sambamba na nia njema iliyopo katika kuwapatia wananchi maendeleo. 

Amesema Jeshi la Wananchi ni taasisi muhimu katika kuchangia maendeleo ya nchi, na kwamba vikosi vya (14 na 151 KJ) vimeonyesha mwitikio mzuri wa kushirikiana na wananchi katika jitihada za kujikwamua kimaendeleo. 

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kuhakikisha kuwa linatimiza malengo yake ya kuwapatia elimu pamoja na huduma za afya wananchi wa eneo hilo. 

Katika ziara hiyo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuchangia mifuko 50 ya saraji ndani ya kipindi cha wiki moja, ili kuchangia ujenzi wa skuli hiyo, sambamba na kugharamia mafuta yatakayotumika kwa ajili ya usafishaji wa kiwanja cha michezo kwa watoto katika eneo hilo. 

Mapema Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Eugene Anathory Ruta amesema mafanikio ya skuli hiyo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais aliyoifanya katika skuli hiyo mwezi Juni, mwaka huu. 

Amesema tangu kufanyika kwa ziara ya mwezi Juni, wafadhili kadhaa wamejitokeza kuchangia maendeleo ya skuli hiyo, na kwamba sasa wana mpango wa kujenga skuli za maandalizi na Sekondari ambazo tayari ujenzi wake umeanza hatua za msingi. 

Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha (14 KJ) J.K. Mbwelo amesema maendeleo ya skuli hiyo hailengi kwa wanajeshi pekee bali kwa jamii nzima iliyowazunguka. 

Kwa sasa wananchi wengi wa maeneo ya Machomanne, Wawi na Vitongoji wamekuwa wakipatiwa huduma za matibabu na elimu katika kituo cha afya ya skuli katika kambi hiyo ya Ali Khamis Camp. 

Maalim Seif pia alitembelea skuli ya Sekondari ya Madungu na kuelezea kuridhishwa na maendeleo ya skuli hiyo. 

Wakati huo huo akiwa katika skuli ya Fidel Castro, Makamu wa Kwanza wa Rais amepongeza hatua ya kutengezwa na kujengwa upya kwa skuli hiyo, hatua ambao imeirejeshe hadhi yake ya asili. 

Ameuagiza uongozi wa skuli hiyo kufanya kazi ya ziada, ili kuhakikisha kuwa ubora wa majengo unakwenda sambamba na matokeo mazuri ya wanafunzi katika mitihani ya Taifa. 

Nae Msaidi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Fidel Castro. Khamis Rashid Nassor, amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa tayari wameweka mikakati imara kuona kuwa Skuli hiyo inarejesha hadhi yake ya Kitaaluma. 

Matengenezo hayo makubwa ya skuli hiyo, nyumba za walimu na mabweni ya wanafunzi, pamoja na ujenzi mpya wa jengo la utawala na vyumba vya kusomea, yamegharimu zaidi ya shilingi Bilioni tatu na nusu. 

Aidha katika hali siyokuwa ya kawaida, Maalim Seif aliingia madarasani kuona jinsi walimu wanavyofundisha pamoja na kuangalia ufahamu wa wanafunzi katika skuli za Madungu na Fidel Castro.

0 comments:

 
Top