Harakati za matengenezo na ujenzi wa njia za kupitia ndege wakati wa kuruka, sehemu ya maegesho ya ndege pamoja na ujenzi wa uzio katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliopo Kiembe samaki zimekuwa zikiendelea vyema.

Ujenzi huo unaotarajiwa kukifanya kiwanja hicho kuwa katika hadhi inayokubalika Kimataifa unafadhiliwa kwa pamoja kati ya Benki ya Dunia { World Bank } kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefanya ziara ya kukagua Mradi huo wa ujenzi uliojumuisha kazi tatu zinazokwenda sambamba za njia za kurukia, jengo la abiria pamoja na eneo jipya la maegesho ya ndege kubwa .

Akitoa taarifa fupi ya mradi huo mkubwa Mshauri wa mambo ya Ufundi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Nd. Fredrick Nkya alieleza kwamba mradi huo unatekelezwa kwa kasi kubwa bila ya kuathiri urukaji na utuaji wa ndege sambamba na mazingira ya uwanja wa ndege.

Nd. Fredrick alisema mradi wa ujenzi wa bara bara za kurukia na kutulia ndege pamoja na maegesho ya ndege unaofanywa na Kampuni ya Sogea Satom ya Ufaransa ulichelewa kuanza kama ulivyokusudiwa kutokana na eneo moja la kazi hiyo kuzunguushiwa uzio na kampuni iliyotangulia mwanzo kujenga jengo la abiria.

Alifahamisha kutokana na ufinyu wa maegesho ya ndege katika maeneo yaliyopo hivi sasa yenye mraba wa mita 21,000 mkandarasi wa ujenzi huo amelazimika kujenga eneo la muda lenye mraba wa mita 8,200.

Mshauri huyo wa mambo ya Ufundi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege alieleza kuwa kazi zinazoendelea hivi sasa ni kuandaa na kusafisha kokoto zitakazochanganywa na changarawe ili zitumike kuwekea tabaka la chain.

Nd. Fredrick alisema kazi hizo zinakwenda sambamba usafishaji wa mazingita katika eneo la mradi pamoja na kuziba viraka kwenye bara bara hizo kazi ambayo hivi sasa imefikia asilimia 97%.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliangalia uzio wa uwanja huo unaokaribia kufikia mita 7,850 ambapo tayari kazi hiyo inakaribia asilimia 67% ikibakisha sehemu ya mita 3,840 inayoendelea kujengwa ikiwa bado ni changamoto kutokana na wananchi hawajafanyiwa tathmini ya mashamnba na mali zao kwa ajili ya ulipwaji wa fidia.

Balozi Seif akiangalia harakati za ujenzi wa bara bara na eneo la maegesho ya ndege mbele ya jengo jipya la abiria wanaosafiri na kuingia Nchini ambapo Msimamizi wa ujenzi wa bara bara hizo kutoka Kampuni ya Sogea Satom ya Ufaransa Bwana Bapeno Roberto alisema ujenzi huo unakwenda vizuri bila ya vikwazo vyovyote.

Bwana Sapeno alisema eneo hilo jipya la maegesho ya ndege kubwa linatarajiwa kuanza kutumika mara baada ya kukamilika kwake ifikapo mwezi Febuari mwaka ujao wa 2014.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Zanzibar Ndugu Said Ndombogani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba vipimo vya kitaalamu vimeonyesha jengo jipya abiria lililojengwa hivi sasa limeongezeka kwa mita sita mbele ya maegesho ya ndege.

Nd. Alisema kwa ushauri wa kitaalamu hali hiyo inastahiki kufanyiwa kwa marekebisho ili iendane na vipimo halisi vya viwanja vya ndege vya kimataifa vilivyopo katika maeneo tofauti Duniani.

Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Mamlaka hiyo kuiandikia Serikali barua rasmi ya ushauri na namna ya kukabiliana na mapungufu hayo na kumpata mshauri muelekezi atakayesaidia taaluma ya kiufundi kufanikisha suala hilo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikagua maendeleo ya matengenezo makubwa ya majengo ya Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali yaliyopo Maruhubi Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Dr. Aboud Sheikh Rajab alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba matengenezo ya majengo hayo yamefikia hatua kubwa kwa zaidi ya asilimia 95%.

Dr. Aboud alisema mkandarasi wa matengenezo ya majengo hayo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo katika kipindi cha wiki moja ijayo na baadaye kukabidhisha rasmi kwa Serikali.

Alifahamisha kwamba kazi za ufungaji wa mashine za kiwanda cha Idara hiyo zitaanza mara moja ikienda sambamba na utolewaji wa mafunzo ya matumizi ya mashine hizo kwa wafanyakazi wa idara hiyo.

Akizungumza na Uongozi na Baadhi ya wafanyakazi wa Idara hiyo mara baada ya kukagua majengo hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwatahadharisha wafanyakazi hao kuwa makini wakati wa matumizi ya mashine hizo zilizogharimu fedha nyingi za Serikali.

Alisema Serikali kupitia Wizara husika imepata tabu na shida katika harakati za kuzipata mashine hizo jambo ambalo wafanyakazi hao wa uchapaji wanalazimika kuzitunza ipasavyo mashine hizo.

“ Nyinyi wafanyakazi lazima muwe wa kisasa katika matumizi ya mashine hizo. Sasa kama hamkuwa waangalifu, wadilifu utendaji wenu unaweza ukaleta mtafaruk “. Alisema Balozi Seif.

“ Hizi Mashine lazima muwe wanyenyekevu nazo kwa vile upatikanaji wake umetupa taabu na shida kubwa iliyotusababisha pia kutafuta msaada na nguvu za wafadhili “. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohd alisema changamoto kubwa iliyojichomoza wakati wa matengenezo ya majengo hayo ilikuwa ni upatikanaji wa fedha.

Dr. Khalid alisema hivi sasa wajenzi wa majengo hayo wameshalipwa kwa zaidi ya asilimia 80% na kilichosalia wakisubiriwa kukamilisha kazi zao ni jumla ya shilingi Milioni Mia Nne na Hamsini Milioni { 450,000,000/- }.

Katibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi Seif kwamba Wizara hivi sasa inajiandaa kupeleka mapendekezo Serikalini ili kuifanya Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuwa Shirika linalojitegemea.

Dr. Khalid alifahamisha kwamba uamuzi huo utachukuliwa kwa lengo la kukifanya kiwanda cha mpiga chapa mkuu wa Serikali kiwe na nguvu za kujitegemea katika ushindani uliopo hivi sasa wa kibiashara ndani na nje ya nchi.

Matengenezo makubwa ya majengo ya kiwanda cha idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali Maruhubi pamoja na Mashine zake mpya yamegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni 4,656,000,000/-.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top