Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewasihi watendaji wote wa Taasisi za umma kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi pamoja na kuzingatia maadili ya kazi kwa lengo la kujiepusha na tabia ya ubadhirifu wa aina yoyote wa mali za Serikali.

Amesema Serikali kamwe haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtendaji ye yote atakayebainika kufanya vitendo vyovyote vitakavyokwenda kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Balozi Seif alitoa nasaha hizo wakati akiufunga mkutano wa kumi na tatu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa ina nia thabiti ya kuondosha maovu ya aina zote katika utumishi wa umma, kuimarisha utendaji na uwajibikaji na kuleta ufanisi na tija katika kazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuipa nafasi Serikali kutekeleza mapendekezo waliyoyatoa kwa misingi ya kuaminiana na kushirikiana katika kupiga vita maovu ndani ya utumishi wa umma.

Alieleza kwamba Serikali imepokea mapendekezo ya Kamati Teule kwa moyo mkunjufu na kushukuru Wajumbe wa Kamati zote kwa kuibua hoja ambazo ni muhimu kufanyiwa kazi katika kuimarisha utendaji wa vyombo vinavyohusika.

Balozi Seif aliwaahidi Wajumbe wa Baraza hilo kwamba Serikali itayatekeleza mapendekezo yote waliyoyatoa kwa misingi ya haki na kwa nia ya kuongeza kasi ya uwajibikaji na kuondoa ubadhirifu wa mali za umma.

“ Naamini Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wana imani kubwa na Serikali yao na wanaitakia mema nchi yetu katika kuiletea maendeleo kwa faida ya wananchi ambao ndio wanaowawakilisha katika Baraza hili “. Alifafanua Balozi Seif.

Hata hivyo Balozi Seif alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaelewa kuwa hatua zozote zinazohitajika kuchukuliwa dhidi ya watendaji wanaotuhumiwa kufanya makosa ya jinai ni lazima tuhuma hizo kwanza kufikishwa katika Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Alisisitiza kwamba uchunguzi huo unapokamilika taarifa za wahusika na wahujumu au wabadhirifu hufikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Balozi Seif aliwahakikishia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba Serikali itachukuwa kila juhudi katika kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika Taasisi za umma na kamwe haitowavumilia watendaji wazembe, wababaishaji, wezi na wabadhirifu kuchafua hatua za kuliletea maendeleo Taifa katika kufikia azma ya kuwa na maisha bora kwa wananchi wote ya kuwaondolea umasikini.

Akizungumzia mradi wa Mkonga wa mawasiliano Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali inakusudia kuendelea kutoa taaluma kwa watumishi wa umma na jamii kuhusu matumizi ya ICT ili kujenga jamii yenye muamko na uelewa wa masuala ya mtandao wa mawasiliano kwa maendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa.

Balozi Seif alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa za huduma za mtandao na mawasiliano na hivyo kuongeza ufanisi katika utoaji huduma na uzalishaji.

Alisema hatua ya kuweka miundombinu ya Mkonga wa Mawasiliano inaendelea vyema na hivi sasa kazi zinazofanyika ni kufikisha miundombinu hiyo katika Wizara na Taasisi nyengine mbali mbali za Serikali.

Alieleza kwa upande wa Ksiwa cha Unguja kazi hiyo imekwisha fanyika kwa asilimia 80 ya kazi yote iliyokusudiwa ya kufikisha huduma hiyo muhimu kwa Taasisi 84 zilizochaguliwa katika hatua ya awali wakati kwa upande wa Pemba kazi ya upimaji imeanza na wakati wowote uwekaji wa miundombinu ya mawasiliano itaanza.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar itakuwa imepiga hatua kubwa katika eneo hili la Afrika Mashariki katika masuala ya mawasiliano hatua itakayoiweka Zanzibar katika ramani ya dunia ya kuwa na miundombinu ya ICT yenye uwezo wa kutoa huduma za mawasiliano ya elektroniki katika sekta mbali mbali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizitaja baadhi ya sekta hizo kuwa ni pamoja na afya, biashara, elimu, kilimo pamoja na uendeshaji wa Serikali (e-Government) na mawasiliano katika jamii (e-community).

Akigusia kazi ya uandikishaji wa wapiga kura na uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura inayoendelea hapa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki katika kazi hii inayoendelea kwa amani na utulivu mkubwa, jambo ambalo limeipa nafasi Tume ya Uchaguzi kuendelea na kazi hiyo bila ya usumbufu wowote.

Alisema katika awamu ya mwanzo, kazi ya uandikishaji imekamilika kwa Majimbo 32 ya Wilaya sita za Unguja na Majimbo 6 ya Wilaya nne za Pemba ambapo hivi sasa Tume ya uchaguzi Zanzibar inaendelea na kazi hiyo kwa Pemba na inatarajia kukamilisha kazi hiyo tarehe 4 Novemba mwaka 2013.

Balozi Seif ametoa wito kwa wananchi wa Majimbo 12 yaliyobakia katika Wilaya ya Wete, Chake Chake na Mkoani Kisiwani Pemba kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uandikishaji na uendelezaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walijadili miswaada mine wa Sheria ambayo ni Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria mbali mbali za Ardhi na Mambo Mengine Yanayohusiana na hayo pamoja na Mswada wa Sheria wa kuanzisha Sheria ya Marekebisho ya Usimamizi wa Utoaji wa Leseni za Biashara na Mambo yanayohusiana na Hayo.

Mengine ni Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya Biashara ya Zanzibar Nam. 4 ya 1989 na kuweka Sheria Mpya ya Biashara ili kuimarisha biashara Zanzibar na mambo yanayohusiana nayo pamoja na Mswada wa Sheria ya Kufuta na Kuandikwa Upya Sheria inayohusu Kampuni na Jumuiya nyengine, Kuweka Masharti Madhubuti Zaidi ya Uratibu na Udhibiti wa Kampuni, Jumuiya na Mambo Yanayohusiana na Hayo.

Wajumbe hao pia walipokea na kujadili taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi juu ya utendaji wa Shirika la Umeme (ZECO) na Baraza la Manispaa.

Jumla ya maswali ya msingi 17 na maswali mengine 157 ya nyongeza yameulizwa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kujibiwa na Mawaziri pampja na Manaibu Mawaziri katika Mkutano hujo wa Kumi na Tatu wa Baraqza la Wawakilishi Zanzibar.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kimeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 11 mwezi wa Disemba mwaka 2013 mnamo saa 3.00 za asubuhi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top