Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kukaribisha wawekezaji vitega uchumi kutoka mashirika,Taasisi na Mataifa washirika katika mpango wake wa kuimarisha uchumi wake pamoja na kuongeza pato la Taifa sambamba na ustawi wa Wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Serikali ya Sharja ukiongozwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Mhandisi Rashid Al Leem ambao upo Zanzibar kwa ziara ya siku mbili kuangalia mazingira ya uwekezaji Vitega Uchumi hapa Nchini.

Balozi Seif alisema Zanzibar imeanza harakati za kuujengea uwezo uchumi wake tokea mwanzoni mwa miaka ya 90 kwa kuimarisha miundo mbinu ili kuuwezesha uchumi wa Visiwa hivi kuacha kutegemea zao moja la karafuu.

Alisema hatua hiyo ya Serikali imelenga kutoa fursa zaidi kwa washirika na Taasisi hizo kuunga mkono mpango huo kwa lengo la kuongeza nafasi za ajira kwa kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi.

“ Zanzibar ni eneo safi kimazingira katika masuala ya uwekezaji. Ni eneo na amani, likizunguukwa na mandhari nzuri ambazo muwekezaji anaweza kulitumia kwa uwekezaji wa miradi ya kiuchumi na maendeleo “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Serikali ya Sharjah kwamba Zanzibar pia ina mtazamo wa kuwa na shirika lake ya Ndege katika muelekeo wa kuongeza mapato zaidi.

Alisema Makampuni ya Sharjah kupitia wataalamu wake wana fursa ya kufanya utafiti wa kuingia ubia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uwekezaji wa sekta ya anga ambayo itasaidia kutoa huduma za usafiri ndani ya ukanda wa Mashariki na kusini mwa Bara la Afrika.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Historia ya kibiashara inaonyesha kwamba Zanzibar imekuwa kituo kikuu cha biashara katika karne kadhaa zilizopita hali ambayo inaweza kurejea katika uhalisia wake endapo mipango hiyo itakamilika hapo baadaye.

Aliupongeza Ujumbe huo wa Serikali ya Sharjah kwa uwamuzi wake wa kuangalia mazingira ya uwekezaji hapa Zanzibar suala ambalo linaonyesha ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya pande hizo mbili.

Mapema Kiongozi wa Ujumbe huo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari ya Sharjah Mhandisi Rashid Al Leem alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Sharjah itaongeza ushirikiano wake na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Mhandisi Rashid alisema Serikali ya Sharjah iko tayari kutoa mafunzo mbali mbali kwa vijana wa Zanzibar, kuwekeza katika miradi tofauti pamoja na kuangalia uanzishwaji wa miradi ya pamoja kati ya mashirika na makampuni ya pande hizo mbili.

Alifahamisha kwamba Zanzibar imefanikiwa vyema katika uimarishaji wa miundo mbali mbali inayotoa kichocheo kwa makampuni mbali mbali Duniani kushawishika kutaka kuwekeza miradi yao Nchini.

“ Zanzibar imeendelea vyema na miundo mbinu iliyojiwekea hasa katika sekta za ardhi na huduma za maji zinazotoa ushawishi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya Zanzibar kuwa na hamu ya kutaka kuwekeza Vitega uchumi vyao “. Alifafanua Mhandisi Rashid Al Leem.

Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya Bandari ya Sharjah alieleza kwamba Makampuni yapatayo 12,000 ya Nchi hiyo tayari yameshatia saini mikataba ya kuendeleza miradi katika mataifa tofauti Barani, Ulaya, Marekani, Asia ambapo Sudan iliyomo Barani Afrika imebahatika kupata miradi ya mafunzo tofauti.

Ujumbe huo wa Viongozi Sita wa Serikali ya Sharjah umekuja Nchini kwa mualiko wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed alipotembelea nchi hiyo hivi karibuni.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top