Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema kauli aliyoitoa katika kikao cha Bunge kilichopita alipotakiwa kuthibitisha ushirikishwaji wa Zanzibar katika mchakato juu ya marekebisho ya sheria ya katiba mpya ya Jamuhuri ya mungano wa Tanzania ilikuwa sahihi.

Balozi Seif alitoa Kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu za Chama cha Mapinduzi za Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba kwa nyakati tofauti wakati akiwa katika ziara ya siku mbili Kisiwani humo.

Kufuatia shutuma za upande wa kampi ya upinzani dhidi yake za kudai kwamba amekuruputa katika kutoa kauli hiyo Bungeni Balozi Seif akitoa ufafanuzi kwa mara ya kwanza kufuatia tukio hilo ili kuwatanabahisha wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuufahamu ukweli.

Balozi Seif alisema inashangaza kuona kambi ya upinzani imeibua hoja ya kumtuhumu yeye katika mabadiliko yaliyofanywa na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakisahau kwamba vipengele wanavyovilalamikia vilikuwemo ndani ya rasimu ya awali ya mswaada huo ambao ulichanw a wakati ulipopelekwa kwa wadau kujadiliwa.

“ Acha waendelee kunitukana na kunikashifu mimi hata sitopungua. Lakini wanapaswa kuelewa kwamba nilichokifanya Bungeni ni sahihi kabisa kwa vile kina uchahidi na kumbu kumbu zote zinazothibitisha ushiriki wa Zanzibar katika suala hilo muhimu “. Alifafanua Balozi Seif.

Balozi Seif ambae pia ni makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba mamlaka ya kutunga mswaada wa sheria inakuwa kazi ya Serikali ambayo hushirikisha wataalamu na wadau wa sekta zote kazi ambayo inaishia wakati unapowasilishwa katika Kamati ya Bunge.

Alifafanua kwamba Sheria ya Bunge la Katiba ilifikishwa Zanzibar na kujadiliwa na kufanywa uchambuzi kupitia wadau wa Sekta hiyo waliotoa nyongeza ya baadhi ya vipengele ambavyo vyote vilikubaliwa na Kamati iliyosimamia mswaada huo.

“ Sheria ya mabadiliko ya katiba imehusisha mambo manne makubwa nayo ni kuundwa kwa Kamati ya kukusanya maoni, kutungwa kwa mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Bunge la Katiba na Kura ya maoni mambo ambayo yaliyokubalika na kuridhiwa na pande zote mbili za Muungano. Sasa ugomvi uko wapi ?“. Aliuliza Balozi Seif.

Akizungumzia uimarishaji wa CCM Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwakumbusha Viongozi na wanachama wa chama hicho kisiwa Pemba kuhakikisha kwamba wanajenga chama ndani ya kipindi hichi kinachoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Balozi Seif alisema kazi ya Viongozi wa Chama hicho katika Mikoa na Wilaya ni kuhakikisha kwamba program za ziara za mara kwa mara kuanzia shina, matawi na majimbo zinatekelezwa ipasavyo ili kuamsha ari za wanachama hao.

Alisema ziara hizo ni vyema zikaenda sambamba na uhamasishaji wa ulipaji wa ada za chama utakosaidia kuwepuka ule mwanya unaoutumiwa na baadhi ya Wanachama kutaka kuwalipia ada wanachama hasa katika kipindi cha uchaguzi kwa lengo la kushawishi kuungwa mkono.

Alisisitiza kwamba mwanachama anapoamua kuilipia ada kadi yake anajijengea nguvu za uwezo wa kuwa huru unaompelekea kuepuka kuburuzwa na wanachama wengine wenye tamaa ya uongozi.

“ Kazi iliyopo hivi sasa ni kwa kila mwanachama kujipanga vyema katika kutafuta wanachama ili kupata turufu na nguvu za kukipatia ushindi chama chetu wakati utapowadia wa uchaguzi mkuu “. Aliongeza Balozi Seif.

Akizungumzia kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM aliwataka Viongozi wa Mikoa hiyo kujipanga katika kushajiisha Vijana kujiandikisha katika daftari hilo kwa vile muda wa kufanya hivyo bado upo.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba bila ya kujiandikisha hakutakua na fursa ya kupiga kura jambo ambalo linaweza kuisababishia mazingira magumu CCM Katika uchaguzi mkuu huo ujao.

“ Bila ya kujiandikisha hakuna fursa ya kupiga kura na bila ya kupiga kura maana yake hakuna ushindi. Sasa siri ya yote hayo ni kwa wale vijana wapya kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye daftari hilo la kudumu la wapiga kura “. Alizidi kufafanua Balozi Seif.

Akiupongeza Uongozi wa CCM wa Mikoa yote miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM ya mwaka 2010 Balozi Seif alisema Viongozi hao bado wanapaswa kuwaelimisha Vijana mfumo mzima wa kuendeleza maisha yao.

Alieleza kwa vile mfumo wa ajira kwa vijana umo ndani ya ilani ya chama hicho Viongozi hao wajitahidi katika kuwaandalia mazingira vijana hao katika kuanzisha vikundi vya uzalishaji mali vitakavyosukuma mbele harakati zao za kiuchumi na kupunguza ukali wa maisha.

Balozi Seif aliwataka Viongozi na wanachama hao kuamini kwamba Serikali zote mbili zitaendela kujitahidi katika kuona zinatoa msukumo wa uwezeshaji kwa vikundi vitakavyoanzishwa ili viweze kujiendesha kiuchumi.

Naye Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi Mama Asha Suleiman Iddi aliwatahadharisha Viongozi na wanachama hao kuwepuka tabia ya kuendeleza makundi ndani ya chama hicho.

Mama Asha alisema kwamba tabia hiyo ikiachiwa kuendelea inaweza kudhoofisha nguvu za chama na hatimae kuleta athari katika harakati zake za kujipanga kuelekea kwenye ushindi wa uchaguzi mwaka 2015.

Aliwakata kutembea kufua mbele kuyatangaza maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho kupitia ndani ya Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mapema akitoa Taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi za chama ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba Katibu msaidizi wa CCM Mkoa huo Abdulla Yussuf Ali alisema yapo mafanikio makubwa ndani ya mkoa huo yanayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM

Nd. Yussuf alisema maeneo mengi ndani ya mkoa huo hivi sasa yanaendelea kupata huduma muhimu za lazima kama afya, maji safi, Kilimo pamoja na Mawasiliano ya usafiri wa Bara bara.

Alieleza kwamba shehia nyingi ndani ya mkoa wa kusini Pemba zimebahatika kuwemo ndani ya mradi mkubwa wa maji safi na salama ambao kumalizika kwake utasaidia kuondosha tatizo kubwa la usumbufu wa huduma ya maji iliyokuwa ikivikabili baadhi ya vijiji Mkoani humo.

Akizungumzia Siasa Katibu Msaidizi huyo wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba Nd. Ali Yussuf alisema hali ya kisiasa hivi sasa imekuwa shuwari mkoani humo tokea kuanza kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ulioshirikisha Vyama Vikuu viwili vilivyokuwa vikipingana vya CCM na CUF.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

0 comments:

 
Top