Jamii ya Kiislamu popote pale Duniani inalazima kufanya jitihada za makusudi katika kuona inaendelea kutumia utamaduni wa Kiislam katika muelekeo zaidi wa elimu, mawazo ya maendeleo, biashara, uchumi, siasa, sayansi na utawala kwa lengo la kuuongezea nguvu ya ziada. 

Hatua hiyo itawapa muono wa kweli watu wengi wasiokuwa waumini wa Dini hiyo kuwaondolea shaka kwamba Uislam si kundi la waumini ambao sera zao ni vurugu, ugaidi na uuwaji mawazo ambayo hata baadhi ya Waislam wanachangia bila kuelewa. 

Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal wakati akilifunga Kongamano la Kimataifa kuhusu Historia ya Ustaarabu wa Kiislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Del Est Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

Alisema misikitini mingi siku hizi imekuwa na hotuba za hamasa, jazba , uchochezi na kugeuzwa kama majukwaa ya kisiasa badala ya kutolewa hotuba za ibada na mafunzo ya Kiislam yanayohusu kumuabudu Mwenyezi Mungu na mafundisho yake ya kupenda kufanya mazuri aliyoyaamrisha na kukataa mabaya aliyoyakataza.

Aliwataka wana jamii wa Utamaduni wa kiislamu kutafakari kwa makini athari hii iliyojichomoza ambapo isipozingatiwa na kupatiwa dawa maalum inaweza kumong’onyoa maadili na usaarabu huo wa Kiislamu. 

Alieleza kwamba ipo haja kwa wakati huu kurejeshwa mfumo wa zamani wa kuifanya Misikiti kuwa ni chimbuko la elimu ambapo ilikuwa mwalimu hukutwa amezunguukwa na vitabu mbali mbali akiendelea kutoa elimu ambapo nyumba zao zikijaa baraza kwa kuwa ni sehemu ya Madrassa. 

Alifahamisha kwamba elimu ya dini ilipewa umuhimu wa kipekee ambapo kila mtoto alijengewa mazingira ya kupata taaluma ya dini kwanza ikifuatiwa na ile ya elimu ya dunia.
 
“ Hakukuwa na mtoto ambaye hakuweza kupata elimu. Vyuo (Madrrassa) vilienea kila pembe. Vijijini ilikuwa wazazi wakenda kulima mtoto mdogo anapelekwa chuoni kulelewa na wakubwa zake. Kwa hiyo alianza kupata hisia za elimu akiwa tangu mdogo “.Alifafanua Makamu wa Raiswa Serikali ya Jmuhuri ya muungano wa Tanzania. 

Dr. Bilal alisema kwamba Utamaduni wa Kiislam umepata nguvu kubwa kutokana na msingi wake wa kurithisha vizazi kwa njia ya mashairi, maandiko na tungo tofauti, hivyo si kosa kueleweka kuwa utamaduni huo umejengwa chini ya msingi wa elimu kwa vile chimbuko lake linatokana na Qur’aan na Sira za Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad (SAW). 

“ Mbali na athari zilizojichomoza lakini bado utamaduni wa Kiislam unabaki kuwa ni utamaduni wa Kiislam. Una miko yake, una sifa zake na una matumizi yake. Utamaduni wa Kiislam unaweza kujisifu kuwa umeweza kusaidia ukuaji wa tamaduni nyingi hasa za Ulaya “. Alifafanua Dr. Moh’d Gharib Bilal. 

Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alisisitiza kwamba Ukuaji wa lugha ya kiarabu kuwa ya Kimataifa ya sayansi na uendeshaji Serikali umesaidia kuufanya Uislam uwe kiungo cha maendeleo chini ya msingi wa Quran inayowaagiza waumini kutafuta elimu popote pale na muda wote wa umri wao. 

Amewapongeza waliowaza kufanya kongamano kama hili hapa Zanzibar na hasa wakati huu ambao Uislam unapita katika mitihani mikubwa na kuelezea matumaini yake kutokana na ushiriki mkubwa wa wajumbe utakaotoa maazimio mazuri yatakayosaidia kupeleka mbele Uislam na ustaarabu wake.

Akisoma maazimio ya wana kongamano hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kongamano hilo Dr. Juma Halifa Juma alisema wana kongamano hilo wamependekeza kuendelezwa kwa makongamano hayo kila mara. 

Dr Juma alisema wana kongamano hao walisisitiza umuhimu wa kuandikwa kwa Historia ya Uislamu wa Afrika ya Mashariki na baadaye kuingizwa katika mitaala itakayozingatia mfumo wa sasa wa Sayansi na Teknolojia. 

Walisema umuhimu wa kubadilishana utafiti kati ya waislamu wa Afrika na wenzao wa mabara mengine Duniani unafaa kuzingatiwa vyema ili usaidie kuimarisha kasi ya utamaduni na Dini ya Kiislamu popote duniani. 

Wana kongamano hao wamemshukuru Mfalme Qaboos Bin Said wa Oman kwa uamuzi wa Serikali yake kupitia Taasisi zake kuandaa kongamo hilo lililotoa fura kwa wanafalsafa, wasomi na waumini wa dini ya kiislam kupata kubadilishana mawazo. 

Naye Mwenyekiti wa mamlaka ya kutunza nyaraka na kumbu kumbu ya Qasri Nchini Oman Dr. Hamad Moh’d Al – Dhawian Bin Balqas alielezea faraja yake kutokana na michango mikubwa ya washiriki wa Kongamano hilo hasa wale wenyeji Zanzibar. 

Dr. Hamad alisema utafiti unaonyesha wazi kwamba Afrika Mashariki ni markaz ya kuleta mabadiliko ya butamaduni wa ustaarabu wa Kiislamu hapa ulimwenguni. 

Akimaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Juma Shamuhuna alisema Zanzibar imepata heshima na bahati kubwa ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo jambo ambalo litaijengea historia ndefu katika masuala ya utamaduni wa ustaarabu wa kiislamu Duniani. 

Jumla ya nyaraka 60 zilijadiliwa katika kongamano hilo lililosheheni wataalamu, wasomi, watafiti na hata wanavyuoni wa dini ya Kiislamu kutoka pembe mbali mbali za Dunia. 

Kongamano hilo la pili la Kimataifa la ustaarabu wa Kiislamu likitanguliwa na lile llililofanyika Uganda mwaka 2012 na limeshirikisha Mataifa kumi na saba mbali mbali Duniani likiwa na lengo la kujitanga za Zanzibar katika Nyanja za Utafiti na Taaluma Kimataifa. 

Serikali ya Oman kupitia ushirikiano wa mamlaka ya kumbu kumbu na nyara ya Nchi hiyo ndio iliyoandaa kongamano hilo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA }.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top