Serikali zote Nchini zitaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi kupitia mipango ya maendeleo ziliyojiwekea ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa kupunguza umaskini { Mkuza } katika kuimarisha Sekta ya Elimu, Afya na soko la ajira ili kuweza kukabiliana na kasi ya ongezeko la idadi ya watu hapa Nchini.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizindua chapisho la mgawanyo wa idadi ya watu kwa umri na jinsi kwenye sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Mjini Dar es salaam.

Balozi Seif alisema Serikali italazimika kuziwekea mikakati changamoto za ongezeko kubwa la idadi ya watu Nchini ambazo takwimu imeonyesha wazi kwamba idadi kubwa ya watu nchini ni vijana wa umri mdogo ambapo watu milioni 19.7 sawa na asilimia 43.9 ya watu wote nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.

Alieleza kwamba Takwimu hizi zimefungua macho na masikio kwa kuonyesha hali halisi ya idadi ya watu nchini. Hivyo ameziagiza Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuboresha Sera zilizopo na kutumia takwimu hizo katika kupanga mipango ya maendeleo.

“ Viongozi wa Serikali zetu zote mbili wanapaswa kutumia na kusambaza matokeo haya katika ngazi zote za utawala kwa kutumia lugha nyepesi ambayo inaeleweka kwa watu wengi ili kuwawezesha wadau wote kupanga mipango sahihi ya maendeleo “. Alsisitiza Balozi Seif.

Akizungumzia kundi la vijana Mwenyekiti mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Balozi Seif alisema Idadi ya Vijana ambayo ni milioni 15.6 sawa na asilimia 34.7 ya watu wote endapo itatumiwa vyema inaweza kuongeza uzalishaji na hatimaye kukuza uchumi wa nchi na kupunguza umaskini.

Alifahamisha kwamba Uhamasishaji wa vijana kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali ni mojawapo ya mikakati itakayowekwa katika kuendeleza vijana na Serikali ina mpango wa kuanzisha benki ya vijana ambayo itakuwa ikitoa mikopo nafuu ili kuliwezesha kundi hilo kubwa kuweza kujiajiri wenyewe. 

Balozi Seif alisema kwa kuzingatia rasilimali zilizopo, Serikali ina dhamira ya kuimarisha viwanda na Kilimo kama njia nyingine za kuwawezesha vijana kupata ajira na kuongeza kipato. 

Aliwaasa Vijana kuacha ya tabia ya kungojea kazi za maofisini ambazo hivi sasa zimepungua na badala yake wajiunge na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali ili waweze kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Kuhusu idadi ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 wapatao milioni 2.5 sawa na asilimia 5.6 ya watu wote nchini Balozi Seif alieleza kwamba kundi hili linahitaji huduma maalum kama vile, matibabu, malazi na huduma nyingine muhimu. 

Alidha alifahamisha kuwa Serikali kwa kushirikiana na washirika na Taasisi nyengine itaendelea kuwapatia wazee hao huduma zote muhimu na zile za lazima kulingana na hali ya uchumi utakavyoruhusu.

Akitoa mada kuhusu chapisho la mgawanyo wa watu kwa umri na jinsi Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya taifa ya Takwimu ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Albina Chuwa alisema ongezeko la idadi ya watu katika maeneo ya Miji imezidi mara tano kutoka sense ya mwaka 1967 hadi mwaka 2012.

Dr.Albino Chuwa alisema idadi ya watu waliokuwa wakiishi mijini mwaka 1966 ilikuwa chini ya asilinia 6.8% ikilinganishwa na zaidi ya asilimia 39% ya mwaka 2012 hii ni kuashiria kwamba watu wanaoishi mijini wamefikia asilimia 30% wakiwa wale walioko vijijini inabakia kuwa asilimia 70%.

Alisema takwimu za idadi ya watu iliyopo hivi sasa nchini katika rasilmali watu sio tatizo lakini kinachohitajika zaidi hivi sasa ni kwa wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza pato litakalolingana na idadi halisi ya watu waliopo.

Dr. Albina Chuwa alifahamisha kwamba mipango ya maendeleo ambayo imo katika sera za Serikali zote mbili za Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitajika katika kustawisha maisha ya wananchi hasa vijana ambao ndio walio wengi na nguvu kazi ya Taifa.

Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu na Makazi { UNFPA } Mwakilishi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Mama Maryam Khan aliipongeza Tanzania kwa umakini wake wa kuendesha zoezi la Sensa kwa mafanikio makubwa.

Marya Khan alisema shirika hilo la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa litaendelea kuunga mkono juhudi za Mataifa wanachama wa shirika hilo katika kusaidia mustakabala mwema wa ustawi wa wananchi wa Mataifa hayo.

Mapema Kamishna wa Sensa wa Tanzania Hajat Amina Mrisho Said kwa niaba ya mwenzake wa Zanzibar Mwalimu Haji Ameri aliwanasihi Watanzania kuzitumia vyema takwimu za sense bila ya kuchakachua ili lengo lililokusudiwa la kufanywa kwa sense hiyo lifikiwe vyema.

Hajat Amina alisema Ofisi za Takwimu bado zitaendelea na uchanbuzi katika madodoso yaliyokuwa yakiulizwa wakati wa zoezi zima la sense ya watu na makazi lililofanyika usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti mwaka 2012.

“ Itapendeza kwa watumiaji wa takwimu hizo hasa wale wachumi wataalamu na wana siasa wakazitumia takwimu hizo za maandishi na si vyenginevyo kwa maana ya uchakachuaji “. Alifafanua Hajat Amina Mrisho .

Akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua chapisho hilo la mgawanyo wa idadi ya watu kwa umri na jinsi Naibu Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya Salum alisema Takwimu hizo tayari zimeshaanza kutumika katika Bajeti za Serikali zote mbili Nchini.

Naibu waziri Saada alisema kwamba matokeo hayo tokea kuanza kutumika katika maandalizi ya Bajeti hizo yameonyesha kuwepo kwa mafanikio makubwa katika mipango ya Serikali ya Bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2013/2014.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Dk Mwinyihaji Makame, alisema serikali itahakikisha takwimu hizo zinatimiza malengo ya kujali fedha zilizotumika katika kuziandaa.

Uzinduzi huu wa Chapisho la Mgawanyo wa Idadi ya Watu kwa Umri na Jinsia ni la pili katika mfululizo wa machapisho yanayotarajiwa kutolewa kama ilivyoainishwa katika ratiba ya machapisho ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. 

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top