Uhusiano wa kubadilishana nyaraka za Kihistoria kati ya Oman na Zanzibar unaweza kuwasaidia wananchi wa pande mbili pamoja na watafiti wa masuala ya Kihistoria kuelewa kwa kina maingiliano ya muda mrefu yaliyopo kati ya Wazanzibar na Waoman ambayo yanafanana Kisilka na Kiutamaduni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Viongozi sita wa Serikali ya Oman ulioongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi hiyo Dr. Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema Zanzibar na Oman zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu tokea karne ya 18 ambao umethibitishwa na wataalamu pamoja na watafiti wa mambo ya Kihistoria kutoka vyuo vikuu tofauti Duniani.

Alielezea haja kwa Viongozi na Wananchi wa Oman na Zanzibar kuendelea kushikamana na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya maendeleo yatakayosaidia ustawi wa vizazi vya sehemu zote mbili rafiki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Oman kupitia ushirikiano wa mamlaka ya kumbu kumbu na nyaraka ya Oman na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kwa kuandaa Kongamano la Kimataifa la Ustaarabu wa Kiiislamu kwa Nchi za Mashariki mwa Bara la Afrika.

Balozi Seif alisema uamuzi huo wa kufanywa kwa kongamano hilo hapa Zanzibar umekuja wakati muwafaka kwa wataalamu wa mambo ya Kale kubainisha kwamba Historia ya Uislamu imeanzia hapa Zanzibar.

“ Nimefurahi kusikia kwamba Historia ya Uislamu imeanza Zanzibar. Inaonyesha watafiti wameliona hili kutokana na asilimia kubwa ya wakaazi wa Visiwa vya zanzibar kuwa waumini wa Dini ya Kiislamu sambamba na Utamaduni wake “. Alieleza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri tafiti za Wataalamu wa masuala ya Historia ambazo zitaibuka katika Kongamano hilo zielekezwe zaidi kunufaisha wananchi na waislamu wa ukanda wote wa Afrika Mashariki.

“ Tafiti hizi za Wataalamu wetu wa Kihistoria itapendeza kama zitaendelea kubakishwa katika maktaba zetu ili zisaidie wananchi, waislamu na hata wasomi wetu wa vyuo vikuu vya ukanda wetu wa Afrika Mashariki “. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.

Naye Kiongozi wa Ujumbe huo wa Serikali ya Oman Waziri wa Habari wa Nchi hiyo Dr. Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani alisema ipo haja ya kuendelea kuhifadhiwa kwa Historia iliyopo ya Zanzibar na Oman kwa faida ya vizazi vijavyo.

Dr. Abdulmumin alieleza kwamba upeo wa tabia za watu wa oman na Zanzibar unaolingana ndio unaochangia na kushawishi wageni na watalii wa mataifa mbali mbali duniani kupendelea kuzitembelea nchi hizi zinazofanana kiutamaduni.

Waziri huyo wa Habari wa Oman alifahamisha kwamba Kongamano hilo la ustarabu wa Kiislamu linalofanyika hapa Zanzibar mbali ya utafiti uliopatikana lakini pia litafungua uhusiano katika Nyanja nyengine za maendeleo kwa nchi shiriki.

Dr. Abdulmumin alielezea faraja yake kutokana na umuhimu wa udugu uliopo kati ya watu wa Oman na Zanzibar ambao umepelekea waoman wengi kujitokeza kushiriki kwenye kongamano hilo.

Alifahamisha kwamba ipo ishara ya kuendelea kwa ziara za mara kwa mara kati ya watu wa pande hizo mbili.

Kongamano hilo la siku tatu linalofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Della East Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kushirikisha Mataifa yapatayo 17 lina lengo la kuitangaza Zanzibar katika Nyanja za utafiti na Taaluma Kimataifa.

Hilo ni kongamano la Pili la Kimataifa la Ustarabu wa Kiislamu kufanyika likitanguliuwa na lile la mwaka 2012 lililofanyika Nchini Uganda na kutolewa uamuzi wa kongomano linalofuata kufanyika hapa Zanzibar kutokana na Historia yake iliyopo sambamba na uhusiano wa karibu iliyonayo na Mataifa ya Kiarabu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top