Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Jumuiya za Chama cha Mapinduzi zinaweza kuendelea kuwa na migogoro iwapo Viongozi na wanachama wenyewe watakubali kuruhusu makundi na mgawanyiko ndani yao.

Kauli hiyo alitoa katika kikao maalum cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa chama cha Mapinduzi { UVCCM } kilichokutana katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar, kwa ajili ya kuridhia na kupitisha Jina la Ndugu Sistus Mapunda aliyependekezwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwa Katibu Mkuu Mpya wa UVCCM.

Balozi Seif alisema Viongozi wanaojaribu kuleta makundi ndani ya jumuiya na Chama chenyewe ni dhaifu na husababisha ufa ndani ya jumuia hizo ambazo ndio tegemeo kubwa la uimara wa chama chenyewe.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa Viongozi hao kufuata Katiba, Kanuni na Utaratibu wa Chama wakielewa kwamba wanalinda heshima kwa wale waliowachagua kushika nyadhifa hizo.

Alisema wapo baadhi ya viongozi waliopewa madaraka kupitia nguvu za wanachama na kuyatumia vibaya madaraka hayo kwa kuendeleza ufidhuli dhidi ya wale wanaowaongoza.

“ Kiongozi lazima awe na heshima kwa wale waliomchaguwa badala ya kuendelea kuwafanyia ufidhuli unaochangia kuzorotesha nguvu za Chama na hata kufikia hatua ya kutoa maamuzi bila ya ushiriki wa wahusika wote “. Alisisitiza Balozi Seif.

Akizungumzia suala la ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha na mali za Jumuiya na Chama chenyewe Balozi Seif alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wanaotumia vibaya fedha hizo.

Aliagiza viongozi na wahusika hao kuhakikisha kwamba mapato yanayopatikana katika vianzio vya Jumuiya na Chama hicho lazima yanaendelea kutumika kwa busara katika kuimarisha miradi na kazi za chama.

Alieleza kwamba yapo matatizo yaliyowahi kuripotiwa kutoka kwa baadhi ya watendaji wa Jumuiya hizo kutumia vibaya fedha na mali za Jumuiya na chama kwa jumla.

“ Ukitaka ugomvi na katibu wako jaribu kuuliza utaratibu wa matumizi ya fedha zinavyotumika. Na ujue kuwa umeshajitafutia balaa kwani Katibu huyo hakusemeshi tena na daima utakuwa adui dhidi yake “. Alifafanua Balozi Seif.

Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Taifa { UVCCM } Sadifa Juma Khamis alitahadharisha kwamba Kiongozi au Mwanachama ye yote asiyekubali kukosolewa au kushauriwa daima atabakia kuwa punguani.

Mwenyekiti Sadifa alisema kazi kubwa ya Umoja wa Vijana wa CCM ni kusaidia kuondoa uonevu, unyanyasaji na ubaguzi inayofanyiwa jamii pahali popote pale hapa Nchini.

Akikuzungumzia uimarishaji wa Jumuiya hiyo Mwenyekiti Sadifa alieleza kwamba Umoja huo umejipanga kurejesha utaratibu wa zamani wa kuwa na Makatibu wasaidizi wa Mikoa na Wilaya kwa baadhi ya maeneo ili kuimarisha nguvu ya jumuiya hiyo.

Alifahamisha kwamba kazi hiyo inatarajiwa kwenda sambamba na utaratibu wa kuwaandaa Vijana kuwa viongozi makini wa hapo baadaye kwa vile wao ndio wenye nguvu za kusimamia sera, siasa na itikadi ya chama.

Akitoa shukrani zake katika Kikao hicho Maalum cha Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake wa utumishi Martin Shigela aliwaasa vijana hao kuheshimu kanuni na miongozo ya Jumuiya na Chama ili kufanya kazi zao kisheria.

Martin Shigela alisema mafanikio yoyote anayoyapata Kiongozi au mwanachama aliyepewa wadhifa hupatikana iwapo muhusika huyo atazingatia taratibu na muongozo aliyopewa.

Katibu Mkuu huyo mstaafu wa UVCCM aliwashukuru Viongozi na Wanachama wa Umoja huo kutokana na ushirikiano waliompa na kupelekea kufanikisha kazi aliyopewa na Chama kwa ufanisi na makini zaidi.

Katibu Mkuu Mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Taifa Ndugu Sistus Mapunda alikuwa katibu wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro pamoja na pia kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya chama cha Mapinduzi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top