Zanzibar itaendelea kuwa mshirika mkubwa na Jamuhuri ya Watu wa China katika kuungwa mkono kwake kwenye harakati za kujiletea maendeleo ya Kiuchumi, kibiashara sambamba na ustawi wa jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Chen Qiiman anayekaribia kumaliza muda wake wa utumishi hapa Nchini.

Balozi Seif ameipongeza Serikali ya China kupitia Balozi wake mdogo hapa Zanzibar kwa juhudi zake za kuunga mkono na kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar.

Alisema Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa mfano katika jitihada za kuunga mkono nchi changa duniani asilimia kubwa ikiwa nchi zilizomo ndani ya Bara la Afrika katika kusaidia taaluma kwenye masuala ya utawala, Uchumi na Maendeleo.

Balozi Seif alitolea mfano wa jitihada hizo za china hasa hapa Zanzibar kuwa ni ule wingi wa miradi ya maendeleo pamoja na majengo tofauti ya Ofisi za umma yanayoendelea kujengwa na wahandisi mbali mbali wa Makampuni ya China.

“ Miradi ya elimu iliyofadhiliwa na China hapa Zanzibar katika ujenzi wa skuli za sekondari mbili na nyengine moja ikiwa katika hatua za kukamilika Unguja na Pemba samba mba na zile Yuan Milioni 1,000,000 za China zilizonunuliwa madeski 400 ni ushahidi wa wazi wa jinsi nchi hiyo ilivyoamua kwa dhati kuunga mkono nchi rafiki “. Alifafanua Balozi Seif.

“ Msaada huu wa wenzetu wa China umetuwezesha kupunguza tatizo la madeski ambapo bado Zanzibar inakabiliwa na uhaba wa vikalio maskulini vipatavyo 25,000 Unguja na Pemba “. Alisisitiza Balozi Seif.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiomba China kuangalia uwezekano wa Makampuni ya Nchi hiyo kufikiria kuwekeza tena katika sekta ya viwanda hapa Zanzibar.

Alisema China ilikuwa nchi ya mwanzo kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa kuwekeza viwanda mbali mbali vilivyosaidia uchumi wa Zanzibar.

Balozi Seif alifahamisha kwamba viwanda hivyo mbali ya mapato ya serikali lakini pia vilichangia kutoa ajira kwa kundi kubwa la wananachi wa Zanzibar hasa Vijana.

“ Vijana wetu wengi walikuwa na ajira za kuendesha maisha yao kupitia miradi kadhaa ya viwanda vilivyoanzishwa na marafiki zetu wa china kama vile kiwanda cha sukari, mahonda, ngozi na viatu Mtoni na kile cha sigareti Maruhubi lakini vyote hivi sasa vimekufa na kuongeza wimbi kubwa la watu wasio na ajira “. Alifafanua Balozi Seif.

Naye Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Chen Qiiman alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Nchi yake itaendelea kutoa fursa za masomo katika fani mbali mbali sambamba na kusaidia miradi ya maendeleo hapa Nchini.

Alifahamisha kuwa Wazanzibar wapatao 700 tayari wameshapata mafunzo ya muda mfupi, muda mrefu na semina mbali mbali ndani ya kipindi cha miaka miwili Nchini China kitendo ambacho kitazidisha kasi ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Balozi Chen Qiiman alisema licha ya kumaliza muda wake wa utumishi lakini Nchi hiyo kupitia uongozi mwengine utakaosimamia shughuli za Diplomasia hapa nchini bado unafikiria njia zaidi za kusaidia maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar.

Alieleza kwamba ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Shein Nchini China katika miezi ya hivi karibuni imechangia kuamsha ari ya makampuni mengi nchini humo kutaka kuwekeza vitega uchumi vyao Zanzibar.

Balozi Chen alisisitiza kwamba ujumbe wa Viongozi na wataalamu 20 kutoka Jamuhuri ya Watu wa China unatarajiwa kuwasili Zanzibar mwishoni mwa mwezi huu kuangalia uwezekano wa kutaka kuwekeza katika sekta za Uvuvi na Utalii hapa Zanzibar.

Balozi huyo mdogo wa China aliyepo hapa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na kwamba miradi ya Zanzibar iliyopata msaada na ufadhili wa Jamuhuri ya Watuy wa China na kuisimamia yeye na watendaji wake mingi imemalizika kwa wakati na ufanisi mkubwa.

Hata hivyo Balozi Chen Qiiman alisema ana matumaini makubwa kwa balozi mwenzake mpya atakayekuja kushika wadhifa huana muelekeo wa kusimamia vyema na kufikia hatua ya kukamilika kwa miradi hiyo.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top