Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za elimu zinazotolewa na vyuo mbali mbali nchini ili kupanda daraja la kitaaluma pamoja na kuwa na uwezo wa uchanganuzi wa mambo tofauti yatakayosaidia Kitaifa katika kupanga na kutekeleza mipango ya kimaendeleo kwa ustadi.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua maabara ya mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano { Tehama } ya chuo Kikuu huria cha Tanzania katika kituo cha Uratibu cha Chuo hicho cha Zanzibar hapo Beit El- Ras Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema jamii imeshuhudia mabadiliko makubwa ya haraka ya sayansi na teknolojia yaliyosababisha baadhi ya wafanyakazi katika taasisi tofauti za umma na hata zile za kibinafsi kuachwa nyuma kwa kutofahamu matumizi ya taaluma hiyo.

Ameuomba uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania uendelee kusogeza fursa hiyo karibu zaidi na wananchi kama ilivyo dhamira ya Chuo hicho katika miaka kumi ijayo ambapo Vituo vya Uratibu kama cha Zanzibar vitabahatika kuwa Chuo kwa kushirikiana na Mikoa husika.

“ Sote tunafahamu kuwa katika miaka ya hivi karibuni, dunia imeshuhudia mabadiliko ya haraka katika matumizi ya Sayansi na Teknolojia. Hii imesababisha baadhi ya wafanyakazi waachwe nyuma kutokana na kutofahamu matumizi ya TEHAMA vizuri “. Alieleza Balozi Seif.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua kuwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimewakomboa wananchi wengi Nchini kwa kuwafikishia elimu ya Cheti, Stashahada, Shahada ya Kwanza pamoja na Shahada za Uzamili na Uzamivu popote pale walipo.

Aliupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Tolly Mbwette kwa azma yao njema ya kuanzisha mafunzo ya TEHAMA hapa Zanzibar kwa ajili ya kusaidia jamii kuendana na kasi ya haraka katika maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba huo ni mpango mzuri utakaowasaidia vijana waliowengi pamoja na wananchi wa kawaida wa Zanzibar kwenda na wakati.

Alielezea matumaini yake makubwa kuwa kwa bidii hii iliyoonyeshwa na chuo hicho, itaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kipindi kifupi kijacho kama yalivyoainishwa katika mpango wa mkakati wa Chuo hicho.

“Bila shaka wengi tumeshasikia kuhusu mkongo wa Taifa wa mawasiliano kwa kutumia kompyuta ambao ujenzi wake unaendelea nchini kote. Mkongo huu unalenga kuunganisha Wilaya zote za Unguja na Pemba na pia kuunganishwa na mtandao wa Kimataifa ambao huunganisha nchi zote duniani. Zoezi hili litakapokamilika thamani na manufaa yake yataonekana endapo tutajua jinsi ya kutumia TEHAMA “. Alifafanua Balozi Seif.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika mpango wake huo kinatarajia kutoa mafunzo ya awali ya matumizi ya kompyuta, Cheti cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano { Tehama } mwaka mmoja na Stashahada ya TEHAMA miaka miwili.

Mapema Mkurugenzi, Kituo cha uratibu cha Chuo Kikuu Huria Tanzania kiliopo Zanzibar Bw. Yussuf Mhangwa alisema kituo hicho kina wanafunzi 451, kati ya hao wanafunzik 267 tayari wameshahitimu masomo yao tokea kuanzishwa kwake.

Bw. Yussuf alisema kazi kubwa iliyopo hivi sasa kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho ni kuwawezesha kupata taarifa mbali mbali zitakazowasaidia kuwapa nguvu na uwezo zaidi wa kukabiliana na masomo yao ya kila siku.

Alisema Kituo cha chuo Kikuu Huria cha Tanzania hapa Zanzibar kikiwa niongoni mwa vituo vya mwanzo kuanzishwa na chuo hicho nchini Tanzania kimekuwa kikitoa mafunzo ya sayansi, sheria, utalii na uchumi katika kiwango cha shahada ya kwanza na ya pili.

Alitoa wito kwa wananchi mbali mbali wa Zanzibar na hasa wale wanafunzi waliomaliza masomo yao ya sekondari kuitumia fgursa hiyo ili kupata taaluma zaidi ya chuo kikuu kwa vile kituo hicho hivi sasa kina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 120 kwa wakati mmoja.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa maabara ya mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwenye kituo cha chuo Kikuu Huria Tanzania Beit El Ras Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Tolly Mbwette alisema lengo lao ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2014 Mikoa Yote Tanzania iwe na Mfumo huo wa Tehama.

Profesa Tolly aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jitihada zake za kuikubali Taaluma hii ya Tehama ambayo pia itasaidia watumishi wa Umma kulingana na muda wao watavyoamua kujipangia.

“ Tumeanzisha kituo cha Jamii katika njia ya kuwawezesha hata wananchi wa kawaida katika sehemu mbali mbali Nchini. Tunba mfano hai kwa wafanyabiashara wadogo wadogo { Maarufu Wamachinga } wanapata mafunzo ya Tehama kwa wakati walioamua kujipangia kuanzia saa 3.00 za usiku hadi saa 6.00 usiku na kwa gharama wanazozimudu “. Alifafanua Profesa Tolly Mbwette.

Makamu Mkuu huyo wa chuo kikuu huria cha Tanzania alifahamisha kwamba jumla ya wanafunzi 67,103 wamepata taaluma na kufaulu mafunzo yao tokea kuanzishwa kwake mwaka 1993 katika ngazi za stashahada na shahada.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top