Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejikita katika kuona mazingira ya uwekezaji sambamba na Vitega Uchumi vya wawekezaji vinalindwa ili viendelee kusaidia pato la Serikali pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wanayovizunguuka vitega uchumivya wawekezaji hao. 

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipotembelea Hoteli ya Paradise Beach Resort iliyopo Marumbi Wilaya ya Kati ambayo imeungua kabisa kwa moto siku mbili zilizopita. 

Balozi Seif alisema Serikali imekuwa ikisisitiza na kuweka mikakati ya miundo mbinu katika eneo la uwekezaji hasa kwenye sekta ya Utalii kwa lengo la kuimarisha nguvu za kiuchumi na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi nchini. 

Akiupa pole Uongozi na wafanyakazi wa Hoteli hiyo ya Paradise Beach Resort kutokana na hasara iliyowapata kufuatia kukumbwa na moto huo Balozi Seif lakini pia akaupongeza Uongozi huo kwa uamuzi wake makini wa kufikiria kuiwekea Bima Hoteli hiyo. 

Alisema ipo miradi mingi ya uwekezaji inayoanzishwa katika maeneo mengi Nchini na hushindwa kuendelea wakati inapopatwa na majanga kama ya moto kwa kukosa kuiwekea Bima ya ajali. 

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizikumbusha Taasisi na mashirika ya uwekezaji kuzingatia ubora wa miradi wanayoanzisha ili iweze kutoa tija kubwa zaidi. 

Mapema Mkurugenzi wa Hoteli hiyo ya Paradise Beach Resort Bwana Egbaert Schoonvelde alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uchunguzi wa chanzo cha moto huo umeanza kuchukuliwa na Taasisi ya Bima ili kuendelea na hatua nyengine ya fidia. 

Bwana Egbaert alimuhakikishia Balozi Seif kwamba licha ya hasara iliyopatikana kutokana na moto huo lakini Uongozi wa Hoteli yake bado una nia ya kuendelea kuwekeza katika masuala ya Utalii hapa Zanzibar. 

Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya utalii hali iliyoufanya uongozi wa hoteli hiyo kushawishika kuwekeza hoteli ya Kitalii hapa Nchini. 

Mkurugenzi huyo wa Paradise Beach Resort alifahamisha kwamba wateja wao wengi ambao wanatokea Nchini Uholanzi wanapendelea kutembelea visiwa vya Zanzibar ili kuona mandhari yake yenye fukwe za kuvutia. 

“ licha ya baadhi ya watu kutulalamikia katika matumizi ya makuti kwenye uwekezaji wa majengo yetu lakini tunafanya hivyo ili kutoa fursa ya kuimarisha utamaduni wa Zanzibar katika matumizi ya Makuti kwenye uwekezaji. Utaratibu huu hata wageni wetu wamekuwa wakiufurahia mno “. Alifafanua Mkurugenzi huyo wa Hoteli ya Paradise Beach Resort Bwana Egbaert. 

Naye Meneja Mkuu wa Paradise Beach Resort Ali Mgeni Mjombo alisema moto huo ambao hadi sasa chanzo chake kimekuwa na utata umeanzia katika eneo la mapumziko liliopo ufukweni mwa Hoteli hiyo { Jet } majira ya saa 10.00 za jioni. 

Ali Mgeni alisema moto huo uliopata kasi kutokana na upepo mkubwa uliokuwa ukivuma katika eneo hilo umesababisha kuungua kwa karibu majengo yote ya Hoteli hiyo ikiwemo minazi pamoja na miti iliyopo pembezoni mwa bara bara karibu na hoteli hiyo. 

Alieleza kwamba Wafanyakazi na Viongozi wa Hoteli hiyo walilazimika kufanya kazi ya ziada katika kusaidia kuokoa maisha na mali za wageni waliokuwa wamepanga kwenye hoteli hiyo. 

Hata hivyo Meneja Mkuu huyo wa Paradise Beach Resort alionyesha kusikitishwa kwake na baadhi ya watu waliofika kusaidia uokozi huo ambao hawakuonyesha uaminifu kwa tabia yao mbaya ya kudokoa vitu na mali za wageni wao. 

Hadi sasa bado haijajuilikana hasara halisi iliyotokana na moto uliounguza Hoteli hiyo ya Paradise Beach Resort ya Marumbi ambayo imekuwa ikitoa huduma za wageni ambao wengi kati yao hutokea Nchini Uholanzi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top