Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe isingependa kuona usalama na amani ya Nchi inapotea kwa kuachwa kuchezewa na baadhi ya watu kwa maslahi yao wakishindwa kuelewa kuwa ni hazina kubwa kwa Taifa zima.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alitoa kauli hiyo mara baada ya kujumuika katika chakula cha pamoja kati yake Familia yake na baadhi ya Wananchi na Viongozi wa Jimbo la Kitope.

Hafla hiyo iliyoshirikisha pia baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa Wilaya ya Kaskazini “ B “ ilifanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya CCM Jimbno la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kasakazini “ B “ Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Balozi Seif alisema zipo nchi nyingi duniani akazitolea mfano Misri na Syriya ambazo ndani ya siku kuu hii ya Iddi el fitri iliyokuja baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa zimezunguukwa na mitutu ya bunduki iliyotanda kuimeza amani waliyokuwa nayo kabla.

“ Ukiipoteza amani ya nchi sharti uelewe kwamba ni tabu na kuirejesha kwake tena inataka kazi kubwa “. Alisisitiza Balozi Seif.

Aliitahadharisha Jamii kuwa macho na baadhi ya watu wanaojaribu kuwashawishi wananchi hasa vijana kupitia misingi ya Dini kuchochea uvunjifu wa amani na utulivu uliopo Nchini.

Balozi Seif amewashukuru wananchi waliojaribu kushawishiwa kujiingiza ndani ya shari katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa msimamo wao usiyoyumba wa kukataa shari hiyo.
Amewaomba wananchi na hasa waumini wa Dini tofauti nchini kutokubali maeneo yao kuchezewa kwa kuoteshwa mbegu mbovu za chuki, uhasama pamoja na shari.

Balolzi Seif aliwakumbusha Vijana kuwa makini katika kujiepusha kutumiwa katika kufanya fujo na maovu kwani kila siku mwanaadamu anapenda kuwa katika mambo mema ikiwemo suala la amani ambalo ndilo la msingi mkuu kuliko yote.

Naye Mke wa Mbunge wa Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliwaasa wazazi kuwa na hadhari na watoto wao ndani kipindi hichi wakati watoto hao wanapoelekea kwenye viwanja vya siku kuu.

Kwa upande wake Katibu Mpya wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini “ B” Subira Mohd Ameir alikipongeza kitendo cha Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif cha kuwa karibu na wananchi wake kwani huleta faraja.

Mapema Balozi Seif akitoa nasaha kwa waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kitope amehimiza suala la kuendelezwa kwa ushirikiano ili kuleta upendo miongoni mwa waumini hao.

Balozi Seif alifahamisha kwamba ushirikiano umekuwa ukisisitizwa kila wakati na kuelezwa ndani ya vitabu vya dini, hivyo waumini hao wanastahiki kuuheshimu na kuufuata.

Siku Kuu ya Iddi El Fitri imekuja kufuatia kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao ni wa Nne katika nguzo tano za Kiislamu ikifuatiwa na Ile ya Hijja kwa muumini mwenye uwezo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top