Serikali imepanga kuhakikisha kwamba matumizi ya teknolojia mbali mbali za kilimo zinatumika ili kufikia malengo yaliyokusidiwa ya kuwa na kilimo cha uhakika, cha kisasa na cha kibiashara. 

Moja ya maeneo hayo ni kuongeza matumizi ya teknolojia zinazohusisha kilimo cha umwagiliaji maji mashambani na katika kutekeleza hilo, Serikali imekamilisha maandalizi na uendelezaji wa skimu 39 zenye jumla ya hekta 16,710 za umwagiliaji kwa njia ya matone.
Makamku wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo katika kilele cha Siku Kuu ya Wakulima Nane nane 2013 zilizokuwa zikifanyika kwa wiki sasa kwenye uwanja wa maonyesho ya Kilimo wa Nzuguni Manispaa ya Dodoma.
Balozi Seif alisema teknolojia hiyo lazima ienezwe kwa wakulima wote nchini kwa kutambua kuwa asilimia 70 ya wananchi nchini Tanzania ni waajiriwa wa sekta ya kilimo kwa sababu ndiyo wanaoishi vijijini.
Alisema kwa upande wa Zanzibar teknolojia hii imesaidia sana ikichukukliwa mfano Mkoa wa Kusini Unguja hasa eneo la Makunduchi ambalo zamani lilikuwa likiagiza ndizi kutoka Wilaya nyingine ambapo kwa sasa kwa kutumia teknolojia hiyo inazalisha ndizi nzuri na kubwa na kuuza sokoni.
Alifahamisha kwamba lengo la Taifa ni kufikia kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kuwa zaidi ya asilimia 6 kwa mwaka ambapo kiwango hicho cha ukuaji kitaiwezesha sekta hiyo kutoa mchango unaotarajiwa katika kuinua uchumi wa Taifa na kupiga vita umaskini.
“ Leo, naona fahari kusema kuwa tumeanza kuona matokeo ya utekelezaji wa mikakati na mipango yetu katika sekta ya kilimo. Hili linajionyesha katika takwimu za ukuaji wa sekta ya kilimo “. Alisisitiza Balozi Seif.
Balozi Seifalisema wakati Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha kuna hakiba ya chakula cha kutosha kuwahudumia wananchi wake wakati wa uhaba wa chakula, wakulima wanahimizwa kuweka hakiba ya kutosha ya chakula katika kaya na wauze ziada tu.
Alisema wapo baadhi ya wananchi hutumia mazao ya nafaka kutengenezea pombe kitendo ambacho si chema na ingefaa kiachwe mara moja ili tuepuke kupata balaa la njaa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba katika kukabiliana na changamoto za kupanda na kushuka kwa bei za mazao ya biashara katika soko la Dunia, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaandaa utaratibu wa kuanzisha Mfuko Maalumu wa Kufidia Bei za Mazao (Price Stabilization Fund) kwa ajili ya kusaidia wakulima pindi bei ya mazao inaposhuka katika soko la dunia.
Balozi Seif ametoa wito kwa Halmashauri za Wilaya kote nchini kuhakikisha vijana wanatengewa ardhi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo na ufugaji.
Alisema kwa uapande Zanzibar Serikali tayari kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili inaendesha mpango kama huu ikishirikiana na Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika.
“ Napongeza kwa dhati vijana wetu walioamua kujiajiri kupitia sekta ya kilimo badala ya kusubiri ajira za maofisini ambazo hazitoshi. Kwa kufanya hivyo, vijana hao wataepuka kutumbukia katika mtandao wa utumiaji wa dawa za kulevya, uzururaji na vitendo vingine viovu. Naiomba Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika iendelee kuwasaidia vijana hawa na kuwatia moyo “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la Ufugaji Balozi Seif alisema ipo haja ya kuongeza idadi ya mauzo ya nyama kutokana na soko la bidhaa ya nyama kuwa kubwa nje ya nchi lakini wafugaji watalazimika wanatza viwango vinavyotakiwa, kama vile usafi na ufugaji mzuri.
Alisema uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 448,387 mwaka 2011/2012 hadi kufikia tani 466,047 mwaka 2012/2013 zikiwemo nyama ya ng’ombe tani 299,581, mbuzi na kondoo tani 115,652.
Aidha alieleza kuwa idadi ya ng’ombe walionenepeshwa imeongezeka kutoka 132,246 kwa mwaka 2011/2012 hadi kufikia ng’ombe 155,206 katika mwaka 2012/2013.
Kwa upande wa ushirika Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inaimarisha sekta hiyo nchini ili kuwawezesha
Alisema mchakato wa kuwa na Tume ya Ushirika uko mbioni kukamilika ili kuweza kuwa na ushirika wenye kutoa huduma bora kwa wanaushirika kote nchini ikiwa imetayarisha mpango maalumu wa kuhakikisha kuwa huduma za ushirika zinaboreshwa kikamilifu kuliko ilivyo sasa.
Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Kilimo Taifa Tanzania { TASO } Bwana Engelbert Moyo alisema sherehe za Nane nane zinalengo la kuwaenzi wakulima na wafugaji Tanzania ambao wana mchango mkubwa kwa Taifa.
Bwana Moyo alisem maonyesho hayo licha ya kutoa huduma mbali mbali kwa wananchi lakini pia hutoa fursa kwa wadau tofauti zikiwemo taasisi za kiserikali na zile za kibinafsi kubadilishana mawazo.
Mwenyekiti huyo wa Chama cha Kilimo Taifa Tanzania alifahamisha kwamba maonyesho ya mwaka huu ya nane nane ymepungua ushiriki wa wazalishaji kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo ya ufinyu wa bajeti.
Hali hiyo imesababisha kupatikana kwa washiriki mia nne tuu kiwango ambacho kiko chini ikilinganishwa navipindi vilivyopita tokea kuanzishwa kwake miaka sita iliyopita.
Akizungumzia katiba mpya Mwenyekiti huyo wa TASO aliishukuru Tume ya mabadiliko ya katiba Tanzania chini ya mwenyekiti wake kwa uamuzi wake wa kuifanya Taso kama Taasisi iliyopewa fursa kuunda mabaraza ya katiba.
Alisema yapo matatizo mbali mbali ndani ya sekta ya kilimo ambayo kupitia mabaraza hayo yameweza kuwasilishwa ili yaingizwe katika katiba mpya likiwemo lile na mgongano wa ardhi ambao umeleta athari kubwa kati ya wakulima na wafugaji na wakati mwengine kufikia hatua ya kusababisha mauaji.
Akitoa salamu katika kilelel cha maadhimisho hayo ya nane nane Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambae ndie Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe hizo Dr. Rehema Nchimbi aliziomba Taasisi zinazohusika na utafiti kutoa majibu ya haraka kuhusiana na suala la matumizi ya mafuta ya ubuyu.
Dr. Rehema alisema kukatizwa kwa matumizi ya mafuta hayo kumetoa mkanganyiko mkubwa kwa wazalishaji wa bidhaa hiyo na kushutumu kuthaminiwa zaidi kwa mafuta yanayotoka nje ya nchi.
Aliiomba Serikali kuandaa mipango maalum ya kuwapatia mizinga ya nyuki wafanyakazi wa taasisi tofauti nchini waliostaafu ili iweze kuwasaidia na kuweza kuendesha maisha yao ya kila siku kwa inaonekana sekta hiyo hivi sasa ni mkombozi mkubwa kwa maisha ya wastaafu hao.
Akimkaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher Chiza alisema Wizara ya Kilimo imepinga dhana ya maonyesho hayo ya kutaka yafanyike kila baada ya miaka mitano badala ya kila mwaka.
Mhandisi Christopher alisema hatua hiyo inaweza kuvuza kazi za wakulima na kutokujuilikana kwa teknolojia mpya za kilimo na mabadiliko mbali mbali yanayojitokeza katika sekta hiyo.
Hata hivyo Waziri wa Kilimo, Mfugo na Ushirika amekishauri Chama cha Kilimo Tanzania { TASO } akuandaa mazingira mazuri yatakayowafanya wakulima kuweza kuyatumia maeneo hayo kuonesha biashara zao bila ya kuwepo kwa gharama zozote zile kwa kufikiria utaratibu maalum utakaokuwa hauwatozi ada za viingilio.
Alisema Serikali itahakikisha inapambana na wachakachuaji wa pembejeo za kilimo kwa kuanzisha sheria ya wahujumu uchumi kutokana na vitendo vinavyoendelea kufanyika kwa baadhi ya wafanya biashara kuamua kuuza bidhaa za kilimo zisizokuwa na kiwango katika masoko.
Akitoa mfano alisema tayari kuna eka 1081 za baadhi ya pembejeo zilizobainika kuwa hazina kiwango na wahusika wameanza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha Waziri wa Kilimo, Mifugo na Ushirika amewaomba Watanzania kujenga utamaduni wa kupenda kula korosho kutoka na kujionyesha wingi wa korosho zinazozalishwa Tanzania zinaliwa nje ya Nchi.
Wizara ya Kilimi, Mifugo na Ushirika ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuona mabadiliko yoyote ya Teknolojia yanayotokea katika Sekta ya Kilimo yanaenda sambamba kwa pande zote mbili za Muungano.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitembelea mabanda mbali mbali kuona bidhaa tofauti zilizozalishwa na kuridhika na hatua iliyofikiwa na wataalamu ndani ya nchi kwa kutumia mali ghafi za hapa Nchini.
Mabanda aliyobahatika kuyatembelea ni pamoja na Mfuko wa chakula wa Kimataifa { WFP } ,Shirika la Kilimo la Kimataifa { FAO }, Kampuni ya Rachi ya Taifa inayojihusisha na masuala ya Ufugaji,kilimo cha umwagiliaji Matunda na zana za Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. 

Mabanda mengine ni Idara ya umwagiliaji maji, banda la Wizara ya Biashara na Viwanda, Banda la Kikosi cha Magereza pamoja na banda la Wizara ya Nishati na Madini.

Ujumbe wa mwaka huu unasema “Zalisha Mazao ya kilimo na Mifugo kwa Kulenga Mahitaji ya Soko”, ikiwa na maana ya kuwa tzizalishwe bidhaa zenye ubora na huku kukiwa na uhakika wa kupata soko. 

Katika Maadhimisho hayo ya sherehe za siku kuu ya Nane nane Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa zawadi kwa washindi bora wa sekta mbali mbali zilizoshiriki katika maonyesho ya maadhimisho hayo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top