Mapinduzi makubwa ya Kiuchumi yaliyofanywa kimahiri na Jamuhuri ya Watu wa China katika miaka ya 80 yamesaidia kuziwezesha nchi nyingi zinazoendelea duniani kupiga hatua zaidi za maendeleo, Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika Tafrija maalum aliyomuandalia Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Balozi Chem Qiman kwa ajili ya kumuaga rasmi akikaribia kumaliza muda wake wa utumishi wa Kidiplomasia hapa Zanzibar.

Tafrija hiyo mahsusi iliyoshirikisha pia baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Serikali na baadhi ya watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanyika katika Hoteli ya Serena Inn iliyopo shangani Mjini Zanzibar na kuambatana na muziki laini uliokuwa ukitumbuizwa na Kikundi maarufu cha kizazi kipya cha Akheri Zamani.

Balozi Seif alisema Mapinduzi hayo ya kiuchumi yya China yametoa fursa kwa watendaji mbali mbali wa taasisi za umma na hata zile binafsi sambamba na jumuiya za uzalishaji katika Mataifa machanga kupata taaluma tofauti Nchini humo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimshukuru Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Chen Qiman kwa umahiri wake ulioimarisha msingi madhubuti wa uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelazimika kumpa heshima kubwa Balozi Chen kutokana na mchango wake mkubwa uliosaidia kuratibu uhusiano wa pande hizo mbili hasa katika masuala ya Taaluma, maendeleo na muelekeo wa miradi ya uwekezaji.

“ Balozi Chen Qiman amefanya kazi kubwa na ya ziada kwa kiwango kisichomithilika cha kusimamia maendeleo ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Jamuhuri ya Watu wa China “. Alielezea faraja yake Balozi Seif.

Akitoa shukrani zake Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Chen Qiman amewapongeza Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa ushirikiano waliompa wakati akitekeleza majukumu aliyopangiwa na Taifa lake.

Alifahamisha kwamba ushirikiano alioupata katika kutekeleza utumishi wake huo umemuwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi na umahiri mkubwa wa hali ya juu.

Balozi Chen alieleza kuwa Ujumbe wa shirika la ndege la China utakaoongozwa na mkurugenzi wake Mkuu baadae unatarajiwa kufanya ziara hapa Zanzibar ili kuangalia mazingira ya kuanzishwa kwa safari za ndege kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Balozi Chen alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande hizo mbili kuwa na usafiri wa uhakika wa moja kwa moja kati ya Zanzibar na kituo cha kimataifa cha Kibiashara cha Nchini china kiliopo katika Jimbo la Guanzhou.

Mapema Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna alimtakia safari njema Balozi Chen ya kuendelea na utumishi wake mpya wa Kidiplomasia katika Ukanda wa nchi za Caribean.

Mh. Shamhuna alisema Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imemteua tena Bibi Chen kuendelea na wadhifa wake huo baada ya kuridhika na kazi kubwa aliyoitekeleza wakati wa utumishi wake hapa Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top