RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya India Mhe. Pranab Mukherjee pamoja na wananchi wa nchi hiyo kwa kutumiza miaka 67 ya uhuru wa taifa hilo.

Salamu hizo za pongezi , zilieleza kuwa yeye mwenyewe binafsi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar zinamtakia heri na mafanikio Rais Mukherjee na wananchi wa Taifa hilo la India.

Pia, salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanatambua uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo kati ya India na Zanzibar, hivyo wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao hao katika kusherehekea siku hiyo adhimu.

Kutokana na hatua hiyo, salamu hizo zilieleza kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo utazidi kuimarishwa kwa kiasi kikubwa kati ya wananchi wa Zanzibar na India kwa lengo la kukuza ushirikiano huo.

Pamoja na hayo, salamu hizo zilipongeza mafanikio makubwa katika sekta mbali mbali za maendeleo yaliopatikana nchini India ambayo yamepatikana kwa juhudi za wananchi na viongozi wao na kusisitiza haja ya kuyaendeleza ili yazidi kuimarika.

Aidha, salamu hizo zilimtakia Rais Mukherjee, heri, afya na uwezo mkubwa wa kuendelea kuliongoza taifa hilo ili lizidi kupata maendeleo zaidi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

0 comments:

 
Top