Mwenyekiti wa Chama cha Mapinzuzi Taifa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuundwa kwa Baraza la ushauri la Viongozi Wakuu wa Chama Cha Mapinduzi ni fursa maalum na nzito itakayosaidia kuimarisha zaidi nguvu ya Chama hicho. 

Dr. Kikwete alisema hayo katika hafla maalum ya uzinduzi wa Baraza hilo linalojumuisha Wenyeviti, Makamu wenyeviti na Makatibu wakuu wastaafu wa Chama hicho iliyofanyika katika viwanja vya Makamu Makuu ya Chama hicho yaliyopo katika Manispaa ya Dodoma. 

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alifahamisha kwamba Wajumbe wa Baraza hilo watakuwa na uwezo kamili wa kushauri hata kuingia katika Vikao vya Juu vya CCM katika masuala mazito yatakayokijengea mustakabala mzuri wa baadae chama hicho. 

Dr. Kikwete alieleza kuwa Uongozi wa CCM ulifikia uwamuzi wa kuundwa kwa Baraza hilo katika Mkutano wake Maalum wa nane Novemba Mwaka 2012 kupitia Ibara ya 127 ya chama hicho baada ya kutambua na kuheshimu mchango wa Viongozi hao. 

Alisema Wana CCM wanastahiki kujipongeza kutokana na ushauri huo ambao uliwahi kupingwa wakati wa nyuma kwa hofu ya Kikundi hicho kutengeneza fitina za kumuingilia Rais katika maamuzi mazito. 

Dr. Kikwete alisema Tanzania imepata mafanikio makubwa kutokana na mabadiliko ya Kiuchumi na hata utulivu wa kisiasa kufuatia mchango wa Viongozi wastaafu ambao kwa sasa watakuwa wakitoa mawazo yao kwa chama kupitia Baraza hilo. 

Dr. Kikwete alimtolea mfano Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mzee Ali Hassan Mwinyi kuwa ni wa kwanza wa mabadiliko ya Uchumi na Siasa ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika miaka ya mwishoni mwa 80 na mwanzoni mwa 90. 

“ Mzee Mwinyi ametuongoza katika mabadiliko hayo ya kiuchumi sambamba nay ale ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa NchinibnTanzania licha ya yeye kutowahi kuufanyika kazi Mfumo huo “. Alifafanua Dr. Kiwete. 

“ Ukweli tuseme mageuzi ya kiuchumi yaliyofanyika Tanzania chini ya uongozi wa Mzee Mwinyi wengine wakimwita Mzee Ruksa mimi ndie niliyeanza kuyafaidi katika kazi zangu za Urais “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. 

Aliongeza kwamba mfumo huo wa kuundwa kwa Baraza la Ushauri la Viongozi wa Wakuu wa Chama Cha Mapinduzi litaondoa usumbufu wa kuwapa tabu wazee hao wa kuitwa mara kwa mara katika Vikao vya Chama kwa lengo la kupata ufumbuzi wa mambo. 

Alisema kwa mujibu wa kanuni za CCM Ibara ya 127 Baraza hilo litakuwa na uwezo kamili wa kushauri hata ndani ya Vikao vya juu vya Chama ama kwa kushiriki wajumbe wote wa baraza au hata uwakilishi wao. 

Mapema Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Abdullrahman Kinana alisema Baraza hilo linalojumuisha Marais wastaafu wa Serikali ya Muungano na Wenyeviti wastaafu wa CCM Taifa Marais wastaafu wa Zanzibar kupitia na Makamu Wenyeviti wastaafu CCM Zanzibar na Bara litafanya vikao vyake kwa mujibu wa utaratibu watakaojipangia wenyewe. 

Katibu Mkuu wa CCM Kikana alisema wajumbe wa Baraza hilo watakuwa na fursa ya kutoa ushauri kwa Serikali zinazoongozwa na Chama cha Mapinduzi Bara na Zanzibar. 

Viongozi hao wanaounda Baraza hilo la Ushauri la Viongozi wakuu wa CCM waliopata fursa ya kuhudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa SMT awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na aliyemfuatia Mh. Benjamin William Mkapa. 

Wengine waliohudhuria ni Makamu mwenyekiti Msaafu na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Amani Abeid Karume pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Mh. Pius Msekwa. 

Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Salimin Amour hakuhudhuria hafla hiyo kutokana na sababu za kiafya wakati Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Phillip Mangula yeye alikuwa na udhuru wa msiba. 

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alibonyeza kitufe maalum kuashiria kuzindua Baraza hilo hafla iliyoambatana na ngoma za vikundi vya utamaduni pamoja na muziki wa kizazi kipya.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top