Kufuatia kuongeza kwa huduma za Kifedha Kitaifa na Kimataifa ndani ya mfumo wa Mtandao wa Mawasiliano wakati umefika kwa Benki ya Posta Tanzania { Postal Bank } kuzidisha juhudi za kufungua matawi yake hasa Vijijini ili kuondosha urasimu kwa wateja wake wanaolazimika kufuatia huduma hiyo katika maeneo ya Mijini.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Uongozi wa Benki ya Posta na kushirikiisha baadhi ya wateja wake iliyofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyopo Migombani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema Wananchi walio wengi katika baadhi ya maeneo hasa vijijini bado wanaendelea kupata usumbufu wa huduma za Kibenki wakati wanapotaka kuhifadhi fedha zao mara wauzapo mazao na bidhaa wanazozalisha mashambani.

Alisema ongezeko la huduma za Kibenki kwa ufunguzi zaidi wa Matawi kwenye makazi yao utatoa fursa zaidi kwa wakulima hao muda mwingi kushughulikia uzalishaji wa miradi yao na kuongeza mapato sambamba na kupunguza umaskini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi na wafanyakazi wa Benki ya Posta Tanzania kwa juhudi zao za kutoa huduma za Kibenki katika maeneo tofauti hapa Nchini wakielewa kwamba mteja kwao ni mfalme.

“ Ucheshi waliokuwa nao watumishi wa Benki ya Posta wakati wanapotoa huduma kwa wateja wao umekuwa kigezo cha mfano kwa taasisi nyengine za Kibenki kwani kinaleta faraja kwa wateja wao na mimi nikiwa mteja wao nilikuwa nikilishuhudia hilo “. Alifafanua Balozi Seif.

Akimkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania Saba Saba Mushingi alisema yapo mafanikio makubwa ndani ya Benki hiyo tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1927 na hivi sasa inajitegemea kwa zaidi ya miaka 12 baada ya mabadiliko ya kisera yaliyotokea mwaka 2001.

Mkurugenzi huyo mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania aliwahakikishia wananchi na wateja wao kwamba Uongozi wa Benki hiyo umezingatia umuhimu wa kuongeza huduma zake na tayari hivi sasa yapo Matawi yasiyopungua 15 ya benki hiyo likiwemo pia lile ya Chake Chake Kisiwani Pemba.

Saba Saba Mushingi alifahamisha kwamba kila Mtanzania ana haki ya kupata huduma za Kibenki na hivi sasa hakuna haja kwa wananchi kuendelea kuweka fedha zao nyumbani kitendo ambacho kinaweza kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Mapema Meneja wa Benki ya Posta Tawi la Zanzibar ambalo ndio mwenyeji wa hafla hiyo Hassan Mohd aliwahakikishia wananchi kuendelea kupata huduma za kibenki katika kiwango kinachoridhisha.

Hassan Mohd alieleza kuwa Jamii imekuwa shuhuda katika utolewaji wa huduma za Western Union ambazo zimekuwa zikifanywa na Benki hiyo tokea mwaka 1999 na kuwapa fursa wananchi kutuma au kutumiwa fedha na Jamaa zao kutoka nchi mbali mbali Duniani.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar