Baraza Kuu la Uongozi
la CUF linakutana jijini Dar es Salaam kwa kikao chake cha kawaida cha siku
mbili.
Akifungua kikao hicho
kinachofanyika ukumbi wa mikutano ofisi kuu ya chama hicho Buguruni Dar es
Salaam, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba amesema pamoja na mambo
mengine kikao hicho kitajadili mpango wa maendeleo kwa wote ulioandaliwa na
chama hicho.
Amesema chini ya
mpango huo, chama hicho kinajipanga kupunguza tatizo la ajira kwa vijana,
sambamba na kuimarisha viwanda vitakavyosaidia kupunguza tatizo hilo
linalowakabili vijana wengi nchini.
Amesema hali ya
uchumi bado ni ngumu kwa wananchi wengi wa Tanzania, hali inayotokana na
kutokuwepo mipango imara ya kukabiliana na tatizo la ajira na matumizi mabaya
ya rasilimali za nchini.
Ametaja tatizo
jengine linaloukabili uchumi wa Tanzania kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za
umma, pamoja na mikataba ya kiuchumi isiyotekelezeka.
Akizungumzi matukio
ya hujuma yanayojitokeza Tanzania, Profesa Lipumba amewaomba Watanzania kuungana
kulaani vitendo hivyo bila ya kujali itikadi za aina yoyote.
Amelilaumu jeshi la
polisi na vyombo vya dola kwa kusahau wajibu wake wa kushughulikia matatizo
makubwa ya kitaifa yakiwemo tatizo la dawa za kulevya, na badala yake
kushughulikia masuala ya kuwadhalilisha wananchi katika maeneo tofauti ya
Tanzania yakiwemo Mtwara, Arusha, Zanzibar sambamba na kuwashugulikia viongozi
wa kidini.
“Kashkashi ya Sheikh
Ponda imekuwa kama ameonekana Osama Bin Laden hapa Tanzania, hii ni hatari
kabisa”, aling’aka Prof. Lipumba.
Mapema akitoa
utangulizi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad
amesema jumla ya wajumbe 46 kati ya 51 wa kikao hicho wamejitokeza, na kwamba
ni halali kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
0 comments:
Post a Comment