Mataifa ya Ukanda wa Bahari ya Hindi yanaweza kuendelea kuwa salama kama ushiriki wa pamoja utazingatiwa ipasavyo katika ulinzi wa mazingira hasa katika vile visiwa vilivyomo kwenye eneo hilo.

Balozi wa Mabadiliko ya Tabia Nchi na Maendeleo ya uhifadhi wa Visiwa Vidogo vidogo anayefanyia kazi zake katika Ubalozi wa Seycheles Umoja wa Mataifa Ronald Jumeau alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Ronald Jumeau alisema Visiwa vingi vilivyomo ndani ya ukanda wa Bahari ya Hindi vimekuwa vikikabilkiwa na changa moto kadhaa hasa zile za uchafuzi wa mazingira ambao unatishia uchumi na ustawi wa Visiwa hivyo.

Alilitaja tatizo moja kubwa linaloathiri visiwa vingi katika eneo hilo kuwa ni ukataji ovyo wa misitu unaotoa mwanya kwa kuyapa kasi kubwa maji ya Bahari kuvamia maeneo ya ardhi.
Balozi huyo wa Mabadiliko ya Tabia Nchi na Maendeleo ya uhifadhi wa Visiwa Vidogo vidogo alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa sekta Binafsi katika visiwa hivyo ambao ni muhimu katika kusaidia uhifadhi ya mazingira ndani ya ukanda huo.
Aliitolea mfano taasisi ya Kimataifa inayopambana na changamoto za mwambao wa Bahari ya Hindi { Indian Ocean Coastal Challenge } {IOCC} ilivyopiga hatua katika kukabiliana na changamoto ndani ya Visiwa hivyo kitaalamu zaidi.

Balozi Ronald Jumeau ambae aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira na Nishati wa Jamuhuri ya Seycheles Bwana Wills Agricole alisema Nchi hiyo imepata mafanikio makubwa katika kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kushirikisha Taasisi binafsi.
Aliishauri Zanzibar kujikita zaidi katika kukabiliana na changamoto hizo za uchafuzi wa mazingira kwa vile tayari imeshalenga kuimarisha zaidi uchumi wake kupitia sekta ya Utalii ambao hutegemea zaidi maeneo ya fukwe na Bahari.
Akizungumzia msiba uliolikumba Taifa la Tanzania kufuatia kuuawa kwa wanajeshi wake saba waliokuwa katika operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani Mjini Dafur Nchini Sudan Balozi Ronaldi Jumeau aliwaomba Watanzania kuendelea kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Alisema Wananchi wa Jamuhuri ya Seycheles wataendelea kuikumbuka Tanzania kwa mchango wake mkubwa wa kusaidia kulinda amani Katika Kisiwa hicho katika miaka ya thamani na kualeta utulivu unaoendelea hadi hivi sasa.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia Ujumbe huo wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona suala la mazingira linaungwa mkono na Jamii yote.

“ Nimepata faraja kutokana na ujio wenu hapa Visiwani nikitarajia kwamba mchango wenu Kitaalamu baada ya kukutana na watendaji wetu utaleta manufaa kwa pande zote husika “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba uchafuzi wa mazingira usipodhibitiwa ipasavyo unaweza kuchangia kutoweka kwa baadhi ya Visiwa katika ukanda huo wa Bahari ya Hindi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top