Zanzibar inahitaji kujengewa uwezo zaidi katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake na watoto zikiwemo unyanyasaji wa kijinsia na ajira kwa watoto.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani, alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).

Amesema vitendo vya unyanyasaji vimekuwa vikiendelea dhidi ya wanawake na watoto jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa maslahi ya taifa na kukuza ustawi wa jamii.

Amesema serikali imekuwa ikichukua juhudi kuwaelimisha wananchi juu ya athari ya vitendo hivyo kwa jamii, na kwamba jitihada zaidi zinahitajika kuweza kuvitokomeza vitendo hivyo.

Amefahamisha kuwa serikali imeweka msisitizo katika elimu kwa watoto, ndio maana imefikia hatua ya kuweza kuwaandikisha watoto wote waliotimiza umri wa kwenda skuli.

Sambamba na hilo amesema serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuwarejesha skuli watoto walioacha skuli kwa sababu mbali mbali zikiwemo umaskini na ajira, hatua ambayo inaonesha kuleta mafanikio.

Hata hivyo amesema sekta ya elimu bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhaba wa madarasa, walimu wa sayansi na mitaala isiyotoa uhakika wa ajira kwa vijana baada ya kuhitimu masomo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UNICEF Tanzania Jama Gulaid, amesema Zanzibar imepiga hatua nzuri katika kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa wanawake na watoto ikilinganishwa na nchi nyengine za Afrika, hasa katika kuzipitia na kurekebisha sheria zinazowahusu watoto.

Gulaid amesisitiza haja ya kulinda afya ya mama na watoto wachanga, kwa kuwashauri akinamama kuwanyonyesha watoto miezi sita mfululizo bila ya kuwapa chakula chengine.

Amefahamisha kuwa hatua hiyo inasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza afya ya mtoto na kumlinda dhidi ya maradhi mbali mbali, sambamba na kuimarisha afya ya mama.

Ameahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa kwa maslahi yao na Taifa kwa jumla.

Katika mazungumzo hayo Gulaid aliambatana na mkuu mpya wa UNICEF Zanzibar, Francesca Morandini.
Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top