Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameuhakikishia umoja wa nchi za visiwa vidogo katika Bahari ya Hindi kuwa, Zanzibar unaunga mkono hatua za kupanua umoja huo pamoja na mipango yake ya kuhifadhi mazingira.

Maalim Seif ameyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka jumuiya hiyo, ulioongozwa na Ronald Jumeau kutoka Sychelees, huko ofisini kwake Migombani.

Ujumbe huo ulifika kwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kumueleza mipango ya mkutano mkuu wa umoja huo uliopangwa kufanyika mwakani huko Samoa.

Maalim Seif amesema mipango ya kulinda mazingira na maliasili za visiwa vidogo haina budi kufanywa kwa mashirikiano miongoni mwa nchi husika na haiwezi kufanikiwa kwa kila nchi kuwa na mipango yake peke yake.

Alisema kwa upande wake, Zanzibar ikiwa kama nchi ya visiwa, inatoa umuhimu wa kipekee katika kulinda mazingira ya baharini na nchi kavu, ili maliasili chache zilizopo ziendelee kulindwa na kuwanufaisha wananchi wake kikamilifu.

Naye, Kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni balozi wa Seychelles nchini Marekani, Ronald Jumeau alisema azma ya umoja huo hivi sasa ni kuzidisha mashirikiano na nchi nyengine za visiwa vidogo, vikiwemo hata vilivyo nje ya Bahari ya Hindi kama vile katika bahari ya Pacific.

Amesema hatua hiyo itaufanya umoja huo kuwa wenye mafanikio zaidi, ambapo pia nchi hizo zitaweza kupata uzoefu mkubwa wa kulinda na kuhifadhi mazingira, na kuwawezesha wakaazi wake kuzitumia maliasili zao kikamilifu na kuziwezesha kuwa endelevu.

Licha ya kuwa Zanzibar inaingia katika umoja huo kupitia Tanzania, imekuwa ikinufaika na miradi mbali mbali ya uhifadhji wa mazingira.

Ujumbe huo pia umekutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej, ambaye ameelezea matumaini yake juu ya Zanzibar inavyoweza kunufaika na umoja huo.

Amesema Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano kuhakikisha kuwa nchi za visiwa zinafanya kazi pamoja na kujifunza mafanikio yaliyofikiwa na nchi nyengine, ili kufikia malengo ya kuwa na maendeleo endelevu.

Amefahamisha kuwa nchi za visiwa ikiwemo Zanzibar zimekuwa zikikumbwa na changamoto kadhaa za kimazingira, ambapo hivi sasa baadhi ya maeneo ya kilimo Zanzibar hayafanyiki kazi kutokana na kuvamiwa na maji ya chumvi, na kuwafanya wakulima wa maeneo hayo kutokuwa na cha kufanya, na kwamba serikali imekuwa ikichukua juhudi kuona kuwa changamoto hizo zinapungua.
Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top