Uongozi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na ule wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } umeshauriwa kuongeza nguvu za ushiriki wa Wizara za Mambo ya Nje na Wizara inayosimamia Utumishi wa Umma katika kuona Chuo cha Taifa cha Ulinzi na Usalama Tanzania kinatekeleza vyema majukumu kiliyopangiwa na Taifa. 

Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohd Gharib Bilal alitoa kauli hiyo wakati akiifunga rasmi Kozi ya mwaka Mmoja ya Wanafunzi 20 kutoka Taasisi za Ulinzi na zile za Utumishi wa Umma Bara na Zanzibar hapo katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania { NDC } kilichopo Kunduchi Wilaya ya Kiondoni Mjini Dar es salaam. 

Dr.Mohd Gharib Bilal alisema ushiriki wa pamoja wa Taasisi hizo utaweza kusaidia kuondosha changamoto zinazokikabili chuo hicho kilichoasisiwa rasmi mwaka mmoja uliopita kwa msaada mkubwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China. 

Alisema muelekeo wa uanzishwaji wa chuo hicho umelenga kuwaandaa Watumishi wa Umma kutekeleza vyema majukumu yao katika misingi ya kitaaluma sambamba na utumishi utaozingatia heshima, nidhamu na uwajibikaji.
Alifahamisha kwamba Taifa limeelekeza nguvu zake katika kuhakikisha linakuwa na Viongozi wazuri katika masuala ya Ulinzi na Utumishi wa Umma uliojaa uwezo wa kutumia maarifa zaidi katika kukabiliana na changa moto zinazojichomoza. 

Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ameupongeza Uongozi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } kwa hatua waliofikia ya kuanzisha chuo hicho. 

Dr. Bilal alieleza kwamba Tanzania ilikuwa ikilazimika kupeleka walinzi na Watumishi wake kupata mafunzo ya juu nje ya Nchi jambo ambalo lilikuwa likilisababishia gharama kubwa na mashaka Taifa. 

“ Chuo hichi ilikuwa ni ndoto na leo hii imekuwa dhahiri kwa vile tayari wakufunzi wake wameanza kufinyanga wanafunzi imara kwa Taifa letu “. Alisisitiza Dr. Bilal. 

“ Nafarajika kuona ule uzinduzi wa wadau wa Chuo chetu nilioufanya Mei Mwaka jana umeanza kutoa mwanga na manufaa kwa Taifa letu “. Aliendelea kufafanua Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Akizungumzia migogoro iliyojichomoza katika baadhi ya maeneo hapa Nchini Tanzania Dr. Bilal alisema inafaa kuangaliwa kwa kina na kitaalamu zaidi na kuwaomba wana chuo hicho kusaidia maarifa katika kuona hali hiyo inafifia au kuondoka kabisa katika mfumo wa amani. 

Alieleza kwamba Taifa linakusudia kukiona Chuo hicho kinakuwa Kitivo cha Taaluma kitakachokuwa na uwezo wa kuhudumia katika Nchi Wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC } pamoja na zile za Kusini mwa Bara la Afrika { Sadec }. 

Aliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa uamuzi wake wa kukubali kusaidia kugharamia ujenzi wa Kampas ya Chuo hicho cha Taifa cha Ulinzi Tanzania { NDC }. 

Mapema Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania { NDC } Luten General Charles Makakala alisema Kozi ijayo inatarajiwa kuwashirikisha wanafunzi wa ziada kumi kutoka Nchi mbali mbali Duniani. 

Kamanda Makakala alisema hatua hiyo imekuja ili kuwapa uwezo zaidi wanafunzi wa chuo hicho katika kumudu vyema mafunzo yao Kimataifa katika fani za ulinzi, Uchumi, jamii sambamba na utafiti. 

Hata hivyo Kamanda Charles Makakala alifahamisha kwamba chuo hicho pia hutoa mafunzo ya Kilimo, utatuzi wa migogoro ya jamii pamoja na masuala ya Mambo ya Nje na uhusiano wa Kimataifa. 

Akimkaribisha Mgeni rasmi Dr. Mohd Gharib Bilal Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Serikali ya Jahumuri ya Muungano wa Tanzania Jop Masima alisema chuo hicho ni sehemu muhimu ya kufinyanga tabia njema za muelekeo wa Viongozi wa Baadae. 

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Bilal alitoa vyeti kwa wahitimu hao 20 wa Kozi ya mwaka Mmoja ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania { NDC } kutoka katika Taasisi za Ulinzi na zile za Utumishi wa Umma Bara na Zanzibar. 

Dr. Bila pia alikabidhi tuzo za Dhahabu na Shaba kwa wanafunzi watatu wa kozi hiyo waliofanya vyema na wale waliokuwa na nidhamu ya hali ya juu ikilinganishwa na wenzao. 

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top