Wakati funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikimalizia kukamilisha kumi la Pili la Maghfira na kuingia kumi la Tatu na la mwisho la kuachwa huru na moto waumini wa Dini ya Kiislamu wanaendelea kushirikiana katika futari za pamoja katika maeneo tofauti hapa Nchini. 

Kitendo hicho cha waumini kinachowakutanisha pamoja katika kufuturu kimesisitizwa ndani ya Quran Tukufu kutokana na umuhimu wake wa kuwajengea umoja na waumini hao kuzidi kushikamana. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi alijumuika na viongoni wa Serikali, Kisiasa , Kidini, Wananchi na baadhi ya waumini wa dini hiyo katika futari ya pamoja kwa mikoa miwili ya Pemba iliyofanyika katika Jengo la Ikulu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar liliopo Tibirinzi Chake chake Pemba. 

Akitoa shukrani kwa niaba ya walioalikwa kwenye futari hiyo iliyoandaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Mmoja wa washiriki hao Sheikh Abdulla Yussuf alisema upo mlingano ulio sawa wa ujira kati ya mwenye kufuturisha na anayefuturishwa. 

Hata hivyo Sheikh Abdulla Yussufu alitanabaisha kwamba mlingano huo hupatikana iwapo jamii ya waumini imetulia katika kufanya ibada zao jambo ambalo mkono wa kheir hunawiri na kuwashukia. 

Sheikh Abdulla liendelea kufahamisha kwamba ucha mungu ulio ndani ya nyoyo za waumini ndio unaosaidia kuongezeka uimarikaji wa hali ya amani, utulivu na upendo miongoni mwa waumini hao. 

Aliwakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi kuzingatia umuhimu wa amani na Umoja ambayo ndio msingi mkubwa wa Dini iliyosisitizwa katika maandiko mbali mbali. 

“ Pahali popote pale penye amani, upendo utulivu na mapenzi miongoni mwa waja wa mola hushusha mkono wa kheir kwa waja hao “. Alifafanua Sheikh Abdulla Yussuf. 

Sheikh Abdulla Yussuf alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa uwamuzi wake wa makusudi wa kuandaa mkusanyiko huo wa kheir uliosaidia kuleta upendo na mahaba kati ya Viongozi na wanaoongozwa. 

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Meja Mastaafu Juma Kassim Tindwa kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewahimiza masheikh na wana vyuoni Nchini kuendelea kuhubiri amani iliyopo. 

Mkuu wa Mkoa Tindwa alisema jamii ya watanzania itaendelea kuifaidi lulu ya amani iliyopo ambayo ni msingi sahihi uliomo ndani ya maamrisho na mafundisho ya dini yenyewe. 

Aliwapongeza Viongozi na wananchi hao kwa ushiriki wao huo na kuacha familia zao kitendo ambacho huleta raha zaidi wakati mfungaji anapokula na familia yake na wakakubali kuridhia mjumuiko huo. 

Ibada ya mwezi mtukufu wa ramadha ni nguzo ya Nne kati ya nguzo tano zinazomuwajikia kila muumini wa dini ya Kiislamu popote pale alipo kuzitekeleza miongoni mwake ikiwemo ile ya Hijja lakini kwa mwenye uwezo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top