Watanzania wameungana pamoja katika kutoa salamu za rambi rambi pamoja na kuwaaga Askari saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } waliouawa Mjini Dafur Nchini Sudan Tarehe 13 Julai mwaka huu baada ya kushambuliwa na waasi wa Nchi hiyo.

Wanajeshi hao wa Tanzania wameagwa rasmi na Watanzania hao wakiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais Dr. Mohd Gharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Makamanda wa Vikosi vya Ulinzi,Mawaziri na Viongozi wa Kisiasa.
Hafla hiyo fupi ilifanyika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Upanga Mjini Dar es salaam na kushuhudiwa pia na Ndugu na Jamaa wa Marehemu askari hao.
Askari hao walioagwa ni pamoja na Sajenti Shaibu Saleh Othman, Koplo Oswald Paul Cahaula, Koplo Mohd Chikilizo Mpandama, Koplo Mohd Juma Ali, Askari Fotunatus Wilbert Msofe, Askari Rodney Geldon Ndunguru na Askari Peter Muhuri Werema.

Akizungumza kwa majonzi na Huzuni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ameuomba Umoja na Mataifa na Umoja wa Afrika kuangalia upya mfumo wa ulinzi unaotumiwa na Majeshi ya Taasisi hizo katika kulinda amani kwenye maeneo mbali mbali Duniani.

Dr. Kikwete alisema marekebisho ya mfumo huo yanaweza kwa kisi kikubwa kupunguza vifo vya askari wa Taasisi hizo wanaoteuliwa kushiriki katika operesheni za majeshi ya kulinda amani ya Taasisi hizo katika mataifa wanachama wa Taasisi hizo ambayo hukumbwa na mizozo ya kivita.

“ Nimepania suala hili kulifikisha katika Vikao vya Umoja na Mataifa { UN } na vile vya Umoja wa Afrika { AU } ili liangalie mfumo unaostahiki kutumiwa hivi sasa ili kupunguza vifo “. Alisisitiza Rais Kikwete.

Alifahamisha kwamba Tanzania imelenga kutetea haki za binaadamu popote pale Duniani tokea ilipopata uhuru wake na ndio maana ikajitokea majeshi yake kusaidia kushiriki katika kulinda amani maeneo mbali mbali Duniani.

Alielezea masikitiko yake kutokana na tukio hilo la kusikitisha na la kuhuzunisha lililoyakumba majeshi ya Tanzania katika ushiriki wa Kimataifa wa kulinda amani ambalo limeleta maumivu miongoni mwa Watanzania walio wengi.

“ Inasikitisha kuona watu wa Dafur wameamua kuwauwa askari wetu mimi naitwa kwa makusudi ambao wamekwenda kuwalinda ili waendelee kuishi kwa amani katika ardhi yao “. Dr. Kikwete alionyesha kukasirika kwake na kitendo hicho.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania amewapongeza ndugu na jamaa wa wafiwa kwa kuwa na moyo wao mkubwa wa uvumilivu kwani msiba huo si wao pekee bali ni wa Taifa kwa jumla.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete alivitaka vikosi vya ulinzi nchini kutokatika tama kutokana na maafa hayo bali wazidishe ari na moyo wa kulitumikia kwa ufasaha Taifa lao.

Alisema Tanzania imepata sifa kubwa katika Nyanja za Kimataifa katika ushiriki wake wa operesheni za kulinda amani kutokana na umakini na umahiri wa askari wake.

Mapema Waziri wa ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Shamsi Vuai Nahodha alisema tukio hilo la mauaji wa skari wa JWTZ Nchini Sudan linaonekana kuwa na mazingira ya mkakati maalum wa vikundi vya waasi wa kuvunja nguvu za majeshi ya Tanzania.
Waziri Nahodha alisema kitendo hicho cha waasi hao chenye dhamira ya kudhoofisha juhudi za Umoja wa Mataifa katika kulinda amani Duniani hakitafanikiwa kamwe.

Mh. Nahodha amezihakikishai familia zilizofiwa na jamaa zao hao kwamba Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaendelea kuwa pamoja na familia hizokatika kuwapa misaada mbali mbali pamoja na kuwahudumia askari waliojeruhiwa ambao wanaendelea kupatiwa matibabu Nchini sudan.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameushukuru Umoja wa Mtaifa kwa misaada iliyotowa katika kukamilisha hatua zote za usafiri wa miili ya wanajeshi hao saba waliouawa Nchini Sudan.

Mapema akitoa Taarifa katika hafla hiyo ya maombolezo Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Meja General Davis Adolf Mwamunyange akielezea tukio alisema askari hao walivamiwa ghafla na waasi hao wakati wakiwa katika kazi za doria.

Kamanda Mwanyunyange alisema gari la walinzi hao lilikwama kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwenye eneo hilo hatua iliyowapa fursa waasi hao kuanza kuwashambulia mashambulizi yaliyodumu kwa takriban saa mbili.

Alisema kikosi hicho cha Tanzania kiliendelea kukabiliana na waasi hao wakiwa na silaha ndog ndogo na kupelekea kutokea kwa mauaji ya askari hao saba na wengine 14 kujeruhiwa mmoja akiwa katika hali isiyo ridhisha.

Katika harakati za kutoa rambi rambi Taasisi na jumuiya mbali mbali zimeanza kuwasilisha michango yao kwa familia za wafiwa ili kuungana nao katika kipindi hichio cha maombolezo.

Taasisi hizo ni Maafisa wa Ulinzi na Watanzania waoishi Nchini Sudan wamejitolewa kutoa Dola za Kimarekani 700, na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Dafur wakajitolea Dola za Kimarekani 1800 wakati Umoja wa Mataifa umetoa Medani Maalum kwa Askari hao kama ishara ya Ushujaa wao.

Akiwasilisha salamu za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Shein kwenye maombolezo hayo Meja Genaral Mustafa Kijuu alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea kwa mshtuko vifo hivyo lakini inaamini kwamba askari hao wamekufa kishujaa.

Dr. Shein alisema msiba huo ni wa Taifa lote na ameitaka Familia za marehemu hao na Majeshi ya ulinzi kuwa na moyo wa sibra wakati Serikali ikiendelea kulifanyia kazi suala hilo na kuahidi kuwa pamoja nao.

Hadi hivi sasa tayari askari 41 wa Nchi mbali mbali zilizoshiriki ulizi wa amani wameshauawa na wengine 55 kujeruhiwa katika operesheni ya Vikosi vya Umoja wa Mataifa Mjini Dafur Nchini Sudan hatua ambayo Tanzania imeamua kuunda Bodi Maalum ya kuchunguza tukio la mauaji wa Askari wake.

Othaman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top