Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema jamii inapaswa kuendelea kuheshimu jukumu la walimu lililowapa dhima ya kujikubalisha kuitekeleza kazi ya Ualimu katika kuwafinyanga watoto ili kuwa na uwezo wa kuongoza ustawi wa Taifa lao hapo baadae.

Balozi Seif alieleza hayo hapo Ofini kwake Vuga Mjini Zanzibar katika hafla fupi ya kuukabidhi Uongozi wa Skuli ya Msingi ya Uzini ya Wilaya ya Kati mashine ya Fotokopi, Meza pamoja na Wino zake ili kusaidia machapisho ya kazi za Skuli hiyo.

Makabidhiano hayo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwaka 2011 wakati akiwa mgeni rasmi kwenye sherehe za kuwazawadia Wanafunzi bora wa darasa la kumi na Moja { Form 1V } wa Skuli hiyo.

Balozi Seif alisema ufinyanzi wa Watoto kitabia, Kimaadili na Kitaaluma ni kazi ya wito na ni ngumu ambayo inahitaji kuungwa mkono na jamii ili iweze kutoa matunda bora ya ustawi wa jamii.

“ Mimi naelewa fika kwamba kazi ya ualimu ni nzito sana na inahitaji subra kwani hata mimi niliwahi kuisomea na hatimae kuifanyia kazi ingawa kwa kipindi kifupi “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Skuli ya Msingi ya Uzini kuhakikisha kwamba mashine hiyo ambayo ni hazina kwao wanaitumia katika mazingira mazuri ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu ujao.

Aliwapongeza walimu na wanafunzi wa Skuli hiyo kwa ustahamilivu wao wa muda mrefu tokea kutolewa kwa ahadi hiyo ambayo ilichelewa kutokana na mawazo yaliyochanganya kufikiria kwamba kilichokuwa kikihitajiwa katika maombi ya skuli hiyo ni kompyuta kumbe ni Fotokopi.

Akitoa shukrani kwa Niaba ya Walimu na Wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Uzini Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Skuli hiyo Tatu Ame Suleiman alisema msaada huo wa Fotokopi umeleta Ukombozi kwao.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Tatu alisema eneo kubwa la Uzini hadi Mchangani lilikuwa likikosa huduma ya fotokopi jambo ambalo lilileta usumbufu hasa kwa walimu na wanafunzi wakati wa vipindi vya Mitihani ya majaribio sambamba na kazi za kila siku ya Kiutawala Skulini hapo.

“ Tunalazimika kutoa shukrani za dhati kwao Mh. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa msaada wako huu na furaha yetu ya kupata mashine hii tunaimani itaenea eneo letu lote la Uzini na Mchangani yake “. Alionyesha furaha yake Mwalimu Tatu Ame.

Naye kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohd Raza Hassan alieleza kwamba kitendo hicho cha msaada wa Mashine ya Fo tokopi mbali ya kuwa cha Kihistoria bali pia kinaongeza ujirani mwema kati ya Wananchi wa Jimbo la Uzini na wale wa Jimbo la Kitope linaloongozwa na Balozi Seif.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Uzini aliushauri Uongozi wa Skuli hiyo kuandaa utaratibu maalum utakaowezesha matumizi bora ya Mashine hiyo na kutoa huduma pia kwa wananachi wengine wa kawaida katika eneo hilo.

Raza alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif kwa umakini wake wa kuendelea kutekeleza Ilani ya Chama hicho kilichopata ridhaa ya Wananchi walio wengi ya kuongoza Serikali.

Mashine hiyo ya Fotokopi, Meza na Wino zake imegharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni 1,500,000/- .

Othman Khamis Ame
Ofisini ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top