Vyombo vya dola vimeshauriwa kutoa fursa sawa kwa vyama vya siasa katika kuendesha shughuli zao za kisiasa, ilkiwa ni hatua moja ya kutekeleza kwa vitendo dhana ya demokrasia nchini.
Ushauri huo umetowa na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika viwanja vya Upenja jimbo la Kitope.
Amesema kila chama cha siasa kilichopata usajili, kina haki ya kuendesha shughuli zake za kisiasa popote Tanzania, bila ya kujali eneo hilo linadhibitiwa na chama gani.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo kufuatia kile alichokiita tabia ya baadhi ya vyama vya siasa kushirikiana na vyombo vya dola kuvinyima haki ya kufanya mikutano vyama vyengine katika baadhi ya maeneo Zanzibar.
"Samahani sana rafiki yangu Balozi Seif, leo nimekuja katika jimbo lako na wala sikuvamia, lakini hii ndio demokrasia inayotakiwa, na wewe nakukaribisha Mtambwe kufanya mikutano, na jimbo langu la uchaguzi ni Mtoni Unguja, njoo ufanye mikutano tafadhali", alisema Maalim Seif.
Alitanabahisha kuwa wakati wa kuvizuia baadhi ya vyama kufanya shughuli zake za kisiasa umepitwa na wakati, na kwamba chama chake hakizuiliki tena kufanya mikutano ya kisiasa pahala popote ndani ya Tanzania.
Katika mkutano huo jumla ya wanachama 435 wengi wao wakitokea shehia ya Mgambo jimbo la Kitope, walijiunga na CUF na kukabidhiwa kadi za chama hicho huku baadhi yao wakirejesha kadi za CCM.
Hassan Hamad.
0 comments:
Post a Comment