Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelenga kuimarisha zaidi miundo mbinu katika Sekta ya Viwanda ili kusaidia Taifa mapato yake pamoja na kutoa ajira kwa kundi kubwa la Vijana wanaomaliza masomo yao. 
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake ya Ujumbe wa Bunge la Oman ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo Bwana Khalid Bin Hilal Ali – Maawal hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 

 
Balozi Seif alisema juhudi hizo zinakwenda sambamba na mipango ya Serikali ya kuifanya sekta ya utalii kuwa muhimili mkuu wa uchumi wa Taifa ambao tayari umeshaanza kuonyesha muelekeo mzuri kimapato. 

 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kazi rahisi kwa sasa ni kuendelea kushawishi Makampuni, Taasisi na hata Mataifa washirika katika kutumia fursa za uwekezaji ndani ya Visiwa vya Zanzibar. 

 
Aliwahakikishia wawekezaji wa Oman kwamba Zanzibar hivi sasa iko katika hali shwari ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita tokea kuanza kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ulioshirikisha Vyama vikuu vya CCM na CUF mara baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. 

 
Alisema maendeleo ya Zanzibar yalikuwa yakilega lega kutokana na mvutano wa kisiasa uliokuwa ukiwayumbisha wananchi walio wengi hali iliyosababisha wananchi hao kukosa kutendewa haki zao. 

 
Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo wa Bunge la Oman kwamba ana matumaini makubwa kutokana na uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Zanzibar na Oman hatua ambayo Serikali ya Nchi hiyo pamoja na wawekezaji wake watatumia fursa hiyo katika kuunga mkono uwekezaji katika sekta tofauti. 

 
Aliipongeza Serikali ya Oman kwa juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mbali mbali ya maendeleo na kiuchumi na akatolea mfano msaada wa sekta ya usafiri na uhuishaji wa kiwanda cha uchapaji Zanzibar kiliopo Maruhubi Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. 

 
Alifahamisha kwamba misaada hiyo kwa kiasi kikubwa ni muendelezo wa uhusiano wa kidamu uliopo kati ya wananchi wa Zanzibar na Oman ambao ni wa kihistoria. 

 
“ Tumepiga hatua kubwa katika uimarishaji wa Kiwanda cha Uchapaji Zanzibar kilichohamishiwa Maruhubi ambacho kinaratibu shughuli zote za uchapishaji za Serikali chini ya msaada wa ndugu zetu wa Oman “. Alisisitiza Balozi Seif. 

 
Naye Mwenyekiti huyo anayeuongoza ujumbe wa wabunge na wataalamu 12 kutoka Bunge la Oman Bwana Khalid Bin Hilal Ali – Maawal amependekeza kuwepo na muendelezo wa ushirikiano kati ya Mabaraza ya Biashara ya Oman na Zanzibar.

 
Bwana Al –Maawal alisema hatua hiyo itazidi kuimarisha uhusiano uliopo wa miaka mingi kati ya pande hizo mbili zinazofanana mila na hata Tamaduni za wananchi wake. 

 
“ Inapendeza kuona Mwananchi wa Oman anapoamua kutembelea Zanzibar anajihisi kama yupo Nyumbani kutokana na muingiliano wa kidamu uliopo kati ya pande hizo mbili “. Alifafanua Bwana Al – Maawal. 

 
Ujumbe huo wa Bunge la Oman uliobeba pia Baadhi ya wataalamu wa sekta za Kibiashara upo Nchini Tanzania kwa ziara rasmi ya kuendeleza uhusiano uliopo kati ya Mataifa hayo kufuatia ziara ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete aliyoifanya Nchini humo mapema mwaka huu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


0 comments:

 
Top