Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewahimiza waislamu kushirikiana na kusaidiana ili kudumisha umoja miongoni mwao.

Amesema umoja na mshikamano ndio nguzo ya kuzidisha mapenzi miongoni mwa waislamu, na kutaka utamaduni huo uendelezwe kwa maslahi wananchi na taifa kwa ujumla.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo alipokuwa akitoa shukrani kwa masheikh na wananchi waliojumuika nae katika futari aliyoiandaa kwa ajili ya viongozi hao wa dini, nyumbani kwake mbweni.

Amewashukuru masheikh kwa kujitokeza kwa wingi katika futari hiyo, na kwamba kitendo hicho kinaashiria mapenzi waliyonayo viongozi wa dini kwa viongozi wao wa kitaifa.

Wakati huo huo Maalim Seif amehitimisha ziara yake ya kutembelea wagonjwa na wafiwa kwa upande wa Unguja, baada ya kufanya ziara katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika ziara hiyo ametembelea maeneo mbali mbali ya Wilaya za Mjini na Magharibi na kuonana na wagonjwa katika mitaa tofauti ikiwemo Mbweni, Tomondo, Magogoni na Mji Mkongwe.

Akiongozana na viongozi mbali mbali wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej na Naibu Waziri wa Elimu Zahra Ali Hamad, Maalim Seif alianza ziara mapema asubuhi katika mitaa wa Mbweni matrekta, Kiembe samaki na Mwanakwerekwe, kabla ya kusitisha ziara hiyo na kujuika katika mazishi ya wanajeshi wawili wa Zanzibar waliofariki Darfur nchini Sudan.

Alihitimisha ziara hiyo kwa kutembelea Jimbo la Mji Mkongwe alipokwenda kuwajuilia hali na kuwafariji mzee Salim Mzee wa Darajani na mzee Ali Yussuf wa Mkunazini.

Ziara kama hiyo inatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Pemba hivi karibuni, ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top