Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kitendo cha kualikana katika futari ya pamoja ni muhimu katika kuimarisha udugu na maelewano katika jamii.

Maalim Seif ameeleza hayo nyumbani kwake Mbweni, baada ya kujumuika na viongozi wa serikali katika futari aliyoiandaa kwa ajili ya viongozi hao.

Amesema utamaduni huo unapaswa kuendelezwa, ili kujenga jamii yenye umoja, mashirikiano na maelewano.

Amewashukuru viongozi hao kwa kuitikia na kuthamini mwaliko huo, na kuwaombea waislamu wamalize mfungo mtukufu wa Ramadhan kwa salama na kupata malipo mazuri ya ibada hiyo.

Viongozi mbali mbali walijumuika katika futari hiyo wakiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis, Mawaziri na Katibu Mkuu Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee.
Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top