Miili saba ya Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } waliouawa baada ya kuvamiwa na waasi wa Dafur Nchini Sudan imefikishwa Nchini Tanzania kwa hatua za mazishi. 
 
Wanajeshi hao wa Tanzania waliokuwa miongoni mwa Vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani Nchini Sudan { UNAMID } wamepokelewa kwa Heshima zote za Kijeshi kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam. 
 
Mamia ya wakaazi wa Mkoa wa Dar es salaam wakiwemo pia ndugu na jamaa wa marehemu hao wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi walishuhudia mashujaa hao walioletwa kwa ndege Maalum ya Umoja wa Mataifa. 
 
Askari hao waliouawa Mjini Dafur Nchini Sudan ni pamoja na Sajenti Shaibu Othman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohd Juma, Koplo Mohd Chikilizo, Askari Rodney Ndunguru, Askari Peter Werema na Askari Fortunatus Msofe. 
 
Wanajeshi hao wa Tanzania wanaotokea Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } iliyopo Mkoani Songea walikuwa katika harakati za kumuokoa askari mwenzao aliyetekwa na waasi wa Sudan. 
 
Hatma ya maisha ya wapiganaji hao wa Tanzania katika Vikosi vya Jeshi la Umoja wa Mataifa Nchini Sudan ilimalizika mara baada ya kuvamiwa kwa mashambulizi na waasi hao yaliyopelekea vifo vyao. 
 
Hata hivyo wanajeshi wengine wa JWTZ waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kikatili wanaendelea na matibabu Nchini Sudan ambapo mmoja kati yao bado yuko katika hali isiyoridhisha.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top