Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Wananchi kujiunga na jumuiya ya wachangiaji Damu Nchini ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma za Damu. 

Wito huo ameutoa katika maadhimisho ya siku ya wachangia damu Duniani zilizofanyika katika Kituo cha Huduma za Damu salama kiliopo pembezoni mwa nyumba za Wazee Sebleni Mjini Zanzibar. 

Balozi Seif alisema kuwepo kwa utaratibu wa kukusanya damu kutoka kwa wachangiaji wa hiari chini ya Mpango wa damu salama kutasaidia kupunguza vifo ambao unakubaliana na dira ya maendeleo ya Milenia ambapo lengo moja wapo ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto. 

Aliiomba jumuiya ya wachangia damu iendelee kuwa ya kudumu na ili kufikia lengo hilo wanachama wake hawana budi kubuni mikakati ya kuingiza wanachama wengi zaidi mjini na vijijini. 

“ Nyinyi ndio benki ya damu na bila ya nyinyi benki hiyo itabakia kuwa ni jiengo lenye wafanyakazi pamoja na mitambo yake, lakini isingekuwa na damu “. Alifafanua Balozi Seif. 

Alieleza kwamba damu ni uhai kwa kiumbe yoyote yule, hivyo kujitolea kwao wachangiaji damu hao kwa hiari kumeonyesha upendo walionao kwa Wananchi wenzao wenye kuhitaji damu hizo. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wachangiaji damu wote kwa moyo wao wa huruma na upendo wanaoendelea kuuonyesha ambao umepelekea kuwepo kwa ukusanyaji mkubwa wa damu Unguja na Pemba unaotia moyo. 

Aliwashauri wafanyabiashara na Taasisi tofauti Nchini kuisaidia Serikali kwa kuziunga mkono huduma za uchangiaji Damu kwa hiari ili kuzifanya huduma hizo zidumu zaidi pamoja na kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje ya Nchi. 

Balozi Seif pia aliwapongeza wapiganaji wa vikosi vya Ulinzi vya Serikali ya Muungano wa Tanzania, vile vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wanafunzi wa Skuli za Sekondari Nchini kwa mashirikiano yao mazuri wanayo toa kwa Kituo cha Damu salama katika kuhakikisha damu ya kutosha inapatikana wakati wote. 

Katika risala yao wana jumuiya ya uchangiaji damu salama { JUWADAHIZ } iliyosomwa na Katibu wao Hamad Bakari Magarawa wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wizara ya Afya kwa juhudi zake za kusaidia jumuiya hiyo. 

Hamad Magarawa alisema jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Damu imekuwa ikiendelea kuishajiisha jamii kujenga tabia ya kukubali kuchangia huduma za damu salama. 

Alisema ushajiishaji huo umesaidia kuibua wimbi kubwa la wachangiaji damu na kufikia mia 850 wakiwa jinsia tofauti Unguja na Pemba kupitia vilabu tofauti hapa Nchini. 

Hata hivyo Hamad Magarawa alieleza kwamba jumuiya hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazochangia kuzorotesha Utekelezaji wa majukumu ya jumuiya hiyo. 

Alizitaja baadhi ya changa moto hizo kuwa ni pamoja na ufinyu wa ufadhili kwa jumuiya hiyo pamoja na baadhi ya watendaji wa sekta ya afya kutokuwa waaminifu kutokana na tabia yao mbovu ya kuuza damu kwa kushirikiana na baadhi ya wachangiaji damu. 

Mapema Meneja Mkuu wa Mpango wa Damu salama Zanzibar Dr. Mwanakheir Ahmed Mahmoud alisema kuzuka kwa maradhi ya ukimwi nchini katika miaka ya tisini kulichangia upungufu wa uchangiaji damu ambao ulikuwa ukifanywa na familia za wagonjwa. 

Dr. Mwanakheir alisema watu wengi walikuwa wakikwepa kuchangia damu kwa kuhofia kudhaniwa kuwa na virusi vya ukimwi na kusababisha usumbufu wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu. 

Meneja Mkuu huyo wa Mpango wa Damu salama alieleza kwamba takwimu zinaonyesha kuwa vifo vingi vilivyokuwa vikiwapata watoto na akina mama vinatokana na upungufu wa damu. 

Akimkaribisha mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya siku ya wachangia damu Duniani Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji aliihakikishia jamii kwamba Wizara hiyo haitovumilia kumchukulia hatua za kinidhamu mtendaji wake ye yote atakayebainika kuwa na tabia ya kuuza damu. 

Wachangiaji damu salama wapatao 850 Unguja na Pemba wamejitokeza kujiunga na vilabu mbali mbali vya uchangiaji damu kupitia Vikosi vya ulinzi vya SMT na SMZ, Wanafunzi wa skuli za Sekondari pamoja na vikundi vya kiraia. 

Baadhi ya wachangiaji damu katika kiwango kikubwa wamepatiwa zawadi maalum katika maadhimisho hayo ambapo Ujumbe wa mwaka huu wa siku ya wachagiaji damu Duniani ifikapo tarehe 14 mwezi Juni ya kila mwaka unaeleza “ Uchangiaji Damu ni zawadi ya Maisha”.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top