Wanamichezo Nchini wametakiwa kuzingatia kanuni ya taratibu za michezo ili ziwawezesha kutekeleza vyema zile sheria 16 za mchezo wa soka sambamba na kujenga mfungamano wa upendo na urafiki miongoni mwao na hatiame kuenea ndani ya Jamii yote kwa ujumla. 

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiyafungua mashindano ya mchezo wa soka ya ZAWEDA Cup yaliyoshirikisha timu 12 za jimbo la kitope pamoja na timu rafiki ambayo yameandaliwa na Jumuiya isiyo ya Kiserikali ya ZAWEDA. 

Balozi Seif alisema Viongozi pamoja na Taasisi tofauti huamua kuanzisha mashindano mbali mbali kwenye maeneo tofauti ili kuwaunganisha pamoja wana michezo pamoja na kuibua vipaji vya Vijana. 

Alisema kinachohitajika zaidi katika Nyanja za michezo ni kudumishwa kwa uanamichezo ambao huleta upendo pamoja na uhusiano mzuri baina ya vikundi, watu na hata mataifa mbali mbali.
Balozi Seif ambae pia ni Mbunge wa Jimbo hilo la Kitope aliwataka wanamichezo hao kudumisha nidhamu katika mashindano hayo ili kulijengea sifa bora jimbo hilo katika Nyanja za michezo. 

Katika kuwahamasisha wana michezo hao Balozi Seif aliahidi kutoa Seti ya TV na king’amuzi chake, Jezi, Kikombe ,mipira pamoja na fedha Taslim shilingi laki 300,000/- kwa Timu ya soka itakayoibuka kuwa mshindi wa kwanza katika mashindano hayo. 

Halkadhalika Balozi Seif akiwahamasisha wana michezo hao pia aliahidi kuwa mshindi wa Pili atazawadiwa Jezi, Mipira na Shilingi laki 150,000/- , mshindi wa Tatu Jezi, mpira mmoja na shilingi 75,000/-. 

“ Nitahakikisha kwamba Timu zote shiriki nitazipatia mpira mmoja. Hiyo itakwenda sambamba na zawadi kwa Mchezaji, Bora, Mfungaji bora na mchezaji mdogo kuliko wote katika mashindano hayo “. Alisisitiza Balozi Seif. 

Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Kitope Makame Mshimba Mbarouk aliwatahadharisha wanamichezo hao kuacha tabia ya kuufanya uwanja wa michezo kuwa sehemu ya masumbwi.

Mshimba alisema tabia za baadhi ya wachezaji kuchukuwa sheria mikononi mwao wakati muamuzi wa mchezo anakuwepo kiwanjani haistahiki kuendelea na inafaa kupiga vita mara moja kwa vile inaondosha heshima ya michezo. 

“ Taratibu za kuendesha michezo na hasa ule mchezo wa soka zimo ndani ya sheria 16 za mchezo huo kimataifa ambazo zinamuajibisha mwanamichezo yeyote aliyejikubalisha kuwemo ndani ya chungu hicho analazimika kuzifuata vilivyo “. Alisisitiza Makame Mshimba. 

Katika Taarifa yao washiriki wa mashindano hayo iliyosomwa na Katibu wa Kamati tendaji wa ZAWEDA Cup Rashid Talib alisema lengo la kuanzisha mashindano hayo yaliyoasisiwa tarehe 16 juni mwaka 2012 ni kuibua vipaji vya vijana katika sekta ya michezo. 

Rashid alisema katika hatua hiyo Jumuiya hiyo inayosimamia mashindano hayo ya ZAWEDA imekusudia kujenga chuo cha mradi wa kuviendeleza vipaji vya vijana ambavyo hatimae vitawapatia fursa za ajira badala ya kutegemea Serikali Kuu. 

Katibu wa Kamati tendaji wa ZAWEDA Cup Rashid Talib kwa niaba ya viongozi wenzake pamoja na wanamichezo hao wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope, Mwakilishi na Kampuni ya Bopar kwa uamuzi wao wa kudhamini mashindano hayo muhimu. 

Katika uzinduzi huo wa ZAWEDA Cup Balozi Seif pia alitoa zawadi za vifaa kwa timu zote 12 zilizokubali kushiriki kwenye mashindano hayo ayanayoingia kwaka wa pili sasa. 

Timu hizo shiriki kutoka Jimbo la Kitope zikikaribisha pia Timu rafiki kutoka wilaya mbali mbali za Unguja ni Mabingwa watetezi wa mashindano hayo Timu ya Soka ya New Star ya Kiwengwa, Kibweni Yourth Organization ya Wilaya ya Magharibi na wenyeji Kitope United. 

Nyengine ni Mahonda Union, Mwache Alale, African Coast, Fujoni Boys, Zaweda, Mahonda Kids, Mgambo Stars, Kilimani City ya Wilaya ya Mjini pamoja na Mbuyuni Stars. 

Katika uzinduzi huo Mbingwa watetezi News Stars ya Kiwengwa waliovalia jezi rangi nyekunda walipambana na Kibweni Yourth Organization katika pambano kali na la kusisimua lililokuwa gumzo kwa walioshuhudia na kuelezea faraja yao kutoka na mchuano huo mkali wa aina yake. 

Matokeo ya pambano hilo lililomvutia mgeni rasmi Balozi Seif akishuhudia pamoja na waalikwa wengine lilimalizika dakika tisini zikiwaacha wababe hao wa New Stars ya Kiwengwa na Kibweni Yourth Organization wakitoa nguvu sawa kwa kufungana goli 2-2.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top