Wadau wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi Zanzibar, wamekutana kwa ajili ya kujadili ripoti ya utangulizi ya utayarishaji wa mpango mkakati wa mabadiliko ya tabia nchi Zanzibar. 

Mpango huo unaotayarishwa kwa mashirikiano kati ya wadau wa mazingira Zanzibar na wataalamu wa mazingira kutoka nchini Uingereza, unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi minne. 

Akizungumza baada ya kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani, mratibu wa mradi wa mazingira na mabadiliko ya Tabia nchi Zanzibar Soud Mohd Juma, amesema lengo la mradi huo ni kuijengea uwezo Serikali kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia nchi.

Amesema mradi huo unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya ufadhili wa mpango wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UN Development Assistance Plan) “UNDAP”, ni muhimu katika kuiwezesha Zanzibar kujiimarisha kiuchumi. 

Amefahamisha kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi zimekuwa zikirejesha nyuma jitihada za serikali za kuimarisha mipango yake ya maendeleo, na kwamba mafanikio ya mradi huo yatasaidia serikali kutekeleza mipango yake kwa ufanisi zaidi. 

Mapema akiwasilisha ripoti ya utangulizi, mtaalamu wa mazingira kutoka nchini Uingereza Paul …. Amesema kuwepo kwa mpango mkakati wa mabadiliko ya tabia nchi ni fursa muhimu kwa Zanzibar kuweza kujitathmini na kuchukua hatua zinazofaa kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. 

Kwa mujibu wa Soud, rasimu ya awali ya mpango mkakati huo inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwezi ujao na baadae kupelekwa kwa wadau wa mazingira nchini kuweza kuitolea maoni.
BY; Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top