Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Awena Sinani Massoud, amewataka wazazi na walezi kuwafunza watoto mila na silka za kizanzibari na kuacha kuiga mila za kigeni ambazo haziendani na maadili ya kizanzibari.

Mama Awena ametoa tahadhari hiyo katika hafla ya maulid ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) iliyofanyika katika Madrasat Swabirina iliyopo Sebleni Wilaya Mjini Unguja .


Amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na vishawishi pamoja na changamoto nyingi ambazo zinaweza kuwatoa watoto katika kufuata maadili yao na kufuata mila za kigeni ambazo zinaweza kuwaingiza katika maangamizi makubwa ya kimaadili.

“Katika nchi hii tunashuhudia jinsi madili katika jamii yanavyoporomoka kwa kiasi kikubwa, vijana na watoto wanaharibika kwa kiwango cha kutisha kutokana na kukosa misingi iliyo bora na usimamizi thabiti kutoka kwa wasimamizi wao katika jamii”, alifafanua Mama Awena na kuongeza,

“Sababu nyingi zimeelezwa kusababisha mambo hayo lakini na sisi wazazi na walezi lazima tukubali kuwa tunalisahau suala la malezi mema kwa watoto na vijana wetu, tunajikubalisha kuwa watumwa wa nchi za Magharibi kwa kuiga mila na tamaduni zao”.

Amefahamisha kuwa utumwa sio ule wa kuuzwa tu bali hata nchi inapopoteza mila na silka zake na kufuata mila za kigeni ni kujiingiza katika utumwa na hatimae kuifanya nchi kuwa katika utumwa.

Ametanabahisha kuwa vijana wengi wamekuwa wakiiga na kukumbatia mambo maovu kwa kisingizio cha utandawazi, na kwamba wazazi wana wajibu wa kuwaelimisha watoto juu ya hasara na faida za utandawazi kwa maslahi yao na taifa kwa jumla.

Ameongeza kuwa watoto wengi hivi sasa wanadharau madrasa na kufuata mambo ya anasa ambayo hayawajengei hatma njema katika maisha yao ya sasa na baadaye.

“Kwa bahati mbaya tuna udhaifu mkubwa kwa vijana wetu kuiga mambo kutoka nje bila ya kujali mataokeo yake, tumekuwa wapokeaji bora wa mambo hasa yale yasiyokuwa na faida bila ya kujua athari zake.

Ameyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na mavazi yasiyo ya stara, anasa na matumizi mabaya ya mitandao.

“Hivi sasa mzazi anashindwa hata kumkana mtoto wa jirani yake imefikia hadi mtaani nyumba zinauza madawa ya kulevya lakini hakuna anaeweza kukemea hadharani jambo hilo na matokeo yake vijana katika mitaa hiyo wanashawishika kujiingiza na taifa kupoteza nguvu kazi ya vijana hao”, alionya Mama Awena.

Amesema kutokana na hali hiyo, jamii haina budi kuwaokoa vijana kutokana na mabadiliko ya Sayansi na teknolojia.

Amesema walimu wa madrasa na skuli nao wana jukumu la kuhakikisha kuwa wanasimamia malezi bora ya watoto wanapokuwa katika maeneo hayo ya taaluma

Mapema Mama Awena alikagua vyumba vya madrasa hiyo na kuona hali halisi ya madrasa hiyo ambayo alisema hairidhishi kukaa wanafunzi wengi, na kuahidi kushirikiana nao katika kutafuta njia ya kutatu tatizo hilo, ili waweze kupata nafasi ya kutosha ya kusomea.

Katika risala yao wana walimu na wanafuzni wa madrasa hiyo walimueleza mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa nafasi ya kusomea pamoja na vitendea kazi vikiwemo vifaa vya kuwekea kumbukumbu vikiwemo Komputa pamoja na vikalio

Madrasa hiyo ilioanzishwa mwaka 1993 ikiwa na watoto 15 ambapo idadi ya wanafunzi iliongezeka hadi kufikia wanafunzi 65.

Na Mauwa Mohd/Hassan Hamad

0 comments:

 
Top