Uimarishwaji wa Miundo mbinu ya Viwanda sambamba na ongezeko kubwa la uzalishaji wa Kilimo ndio njia muwafaka ya kukabiliana na ukosefu wa ajira unayoyakumba mataifa kadhaa machanga yanayoendelea Duiniani.
 
Hayo yalikuwa mawazo na muelekeo wa baadhi ya Viongozi wa Mataifa kadhaa Duniani walioshiriki kwenye majadiliano ya Kimataifa ya ushirikiano kwa manufaa ya wote ukiwa katika siku ya pili unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es salaam.

Waziri Mkuu Mstaafu wa Malaysia Dr. Mahathir muhamad aliuambia mkutano huo wa majadiliano ya Kimataifa kwamba asilimia 70% ya watu wote Duniani hawana ajira hali ambayo inaongeza umaskini hasa katika Mataifa machanga.

Alieleza kwamba nchi changa zinapaswa kujikita zaidi katika miundo mbinu ya viwanda ambavyo uwepo wake hupunguza wimbi kubwa la wananchi wasiokuwa na ajira.

Dr. Mahathir alisema kuna haja kwa mashirika na Taasisi za Kimataifa Duniani kuendelea kuunga mkono msimamo wa Mataifa machanga katika kunyanyua uchumi kwa lengo la kupunguza hali duni za Kimaisha za Wananchi wa Mataifa hayo.

Alisema Taasisi hizo zina mchango mkubwa katika kusaidia kuongeza nguvu za uzalishaji na hatimae kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini uliokithiri katika nchi zinazoendela kujinasua Kiuchumi.

“Msimamo wa Mataifa machanga wa kunyanyua hali za maisha ya wananchi wake unafaa kuunga mkono na Taassi na Mashirika binafsi hasa yale ya Kiuchumi ambayo yana mchango mkubwa katika kusaidia kunyanyua uchumi wa wananchi hao “. Alisisitiza Waziri Mkuu huyo wa Malaysia Dr Mahathir.

Akitilia mkazo suala la umuhimu wa Viwanda Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema mataifa machanga ni vyema yakabadilika ili kuelekea kwenye sekta hivyo ambayo ni muhimumi mkuu unaoongeza kasi ya uchumi Duniani.

Rais Museveni alieleza kwamba kumekuwa na mivutano na misongamano ya umiliki wa ardhi unaotokana na uwiano wa vipato kwa baadhi ya watu katika mataifa mbali mbali maskini hali ambayo husababisha zaidi umaskini.

Alizashauri nchi changa kuhakikisha kwamba zinajinasua katika wimbi la umaskini kwa vile tayari zinajiendesha zenyewe kwa karibu miaka 50 sasa tokea zipate uhuru wake kutoka kwa wakoloni waliokuwa wakihodhi na kusafirisha rasilmali za nchi hizo.

“ Tumekuwa tukishuhudia balaa kubwa kwa baadhi ya mataifa ndani ya bara la afrika wakati wanapofanikiwa kuibua miradi mipya ya kiuchumi hasa inayohusu mafuta na gesi “. Alifafanua Rais Museveni.

Wakitoa taarifa za kitafiti , kiuchumi, kijamii na Kisayansi baadhi ya Wataalamu wa Nchi shiriki wa majadiliano hayo ya Kimataifa ya ushirikiano kwa manufaa ya wote walieleza umuhimu wa Mataifa machanga kujenga miundo mbinu ya teknolojia ya Kisasa katika ngazi za chini.

Profesa Heneri Dzinotyiweyi wa Zimbabwe alisema mfumo huo utazijengea uwezo na nguvu madhubuti jamii katika muelekeo sahihi wa kuingia ndani ya mfumo wa kisasa wa sayansi na Tekonojia mbwembwe.

Naye waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Profesa Makame Mnyaa Mbarawa alisema mawasiliano ya teknolojia yamesaidia kuibadilisha kwa haraka harakati za kila siku za maisha ya jamii.

Profesa Mnyaa alitolea mfano wa mawasiliano ya simu ndani ya bara la Afrika yalivyonyanyua uchumi, ustawi wa jamii kupitia mitandao ya simu ambayo mbali ya kutoa huduma za haraka hasa za kifedha pia zimeweza kutoa ajira kwa kundi kubwa la Vijana.

“ Utafiti wa hivi karibuni umebainisha kuwa zaidi ya watu Milioni 360,000,000 Barani Afrika hivi sasa wanatumia huduma za mawasiliano ya simu sambamba na huduma za kifedha kupitia mitandano hiyo ya simu “. Alifafanua Profesa Mnyaa.

Akiufungua mkutano huo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alisema umefikia wakati kwa mataifa machanga kuona umuhimu wa kuwekeza katika miundo mbinu ya Sayansi na Teknolojia ya Kiuchumi.

Alisema Tanzania tayari imeanza kujiandaa na mfumo huo kwa kuimarisha elimu ya msingi na sekondari hadi chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mandela ambacho kinatarajia kutoa wataalamu wazuri wa fani ya Sayansi na Teknolojia kwa manufaa ya Nchi.

Vile vile alielezea kwamba suala la utafiti katika fani hiyo muhimu serikali ya Tanzania imeamua kutenga fedha kwa vijana wenye vipaji maalum katika kuwajengea uwezo zaidi kwa kuwawezesha kuibua teknolojia ya sayansi itakayoleta nafanikio ya haraka katika Jamii.

Alifahamisha kwamba wapo vijana ambao tayari wameanza kuwekeza katika masuala ya sayansi kwa kubuni mashine za kisasa zinazotoa huduma katika taaluma bora inayokwenda na wakati.

“ Tatizo linalowakabili wakulima walio wengi nchini Tanzania hivi sasa ni kuendelea na jembe la mkono ambalo limepitwa na wakati kutokana na mabadiliko yaliyopo hivi sasa ya sayansi na teknolojia kwa kuangalia zaidi uchumi “. Alisema Dr. Kikwete.

Zaidi ya wajumbe 800 kutoka Nchi mbali mbali Duniani wameshiriki Mkutano huo wa Siku Nne wa Majadiliano ya Kimataifa ya ushirikiano kwa manufaa ya wote.

Zanzibar inawakilishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na baadhi ya Mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali kutoka sekta ya Biashara, fedha na Utawala.

Othman Khamis Ame na Mwantanga Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top