Ndugu Denis,
Mimi natoa maoni yangu lakini najua na wengine wanaweza au kuniunga mkono au kunikatalia. Hiyo ndiyo demokrasia. Ikiwa ninachotetea kikikataliwa na hakuna madhara yatayotokea huko mbele ya safari safi tu. Ikiwa nikishauri kitu watu wakakikataa na baadaye wakadhurika, walau mimi nitasema nilisema na nafsi yangu itakuwa na amani .

Mzee Abeid Karume aliweza akawaongoza Wazanzibari wakakubali ushauri wa Muungano lakini leo wanao viongozi wengine wanaowashauri kutengana kuna masilahi kwa Wazazibari. Kazi kwao kutafakari. Pia Watanzania wa Bara wengine wanadhani Muungano na Zanzibar si lazima lakini mimi nafikiri itakuwa haina usalama sana kwa Tanzania Bara kuwepo Zanzibar yenye kuwa Kuwait ya Afrika Mashariki, yenye jeshi lake linalodhibitiwa na Uingereza na Marekani na labda yenye kuwa na vituo vya kijeshi vya Marekani, huku viongozi wake wakijifanya eti Wazanzibari wote ni Waislamu kama vile wanavyofanya viongozi wa Kuwait au Oman...


Nakumbuka wapo Wazanzibari wengi wenye biashara zao Tanzania Bara na wenye mahusiano ya karibu na watu wa Tanzania Bara yanayosukumwa na ufuasi wa dini moja ya Kiislamu au kupeana mikopo ya kuanzishia biashara..Wote hawa ni WATANZANIA na wanayo haki kumiliki ardhi Tanzania Bara na kujisikia wako nyumbani. Mheshiwa Waziri wa Afya wa sasa aliwahi kuwa Mbunge jimbo moja hapa Tanzania Bara na baadaye karudi Zanzibar na kuchanguliwa Ubunge jimbo la Zanzibar na sasa ni Wazir wa Afya kwenye serikali ya Muungano inayoshughulikia mambo ya afya Tanzania Bara. .Mzanzibari anayedhani kuna manufaa kwa Wazanzibari katika kufuta utaifa wa UTANZANIA nakufufua utambulisho wa Utanganyika sina hakika amekaa na kufikiria sana juu ya madhara ya kufufua utambulisho huo….Labda kama ni Mzanzibari anayeishi Omani au Kuwait kwa sasa na hana mahusiano na Wazanzibari wenzake walio na mahusiano ya karibu na Tanzania Bara.


Vile vile, kiulinzi na usalamana mtengamano kati ya waumini wa dini mbali mbali Tanzania Bara unasaidiwa n akuwepo dola moja la Tanzania . Watanzania Bara wanaodhani ulinzi na usalama wa Tanzania Bara utakuwa wa gharama zile zile kama za sasa ambapo kuna uraia wa Tanzania moja, tuna jeshi la ulinzi, usalam na polisi moja ya dola moja la taifa moja la UMAJUMUI wa KIAFRIKA la Tanzania, lisilo mbagua mtu kwa uzawa wake wala nasaba yake kuhusisha nasaba za Asia au Ulaya, Niinashaka kama kweli hawa wanao shabikia kurudi kwenye utambulisho wa UTANGANYIKA tuliopachikwa na wakoloni wa Kiingereza baada ya sisi kuitwa GERMAN EAST AFRIKA na Wagerumani hadi 1919, wamekaa nakutafakari kwa kina juu ya jambo ili kama alivyo kuwa amefanya Mwalimu Nyerere.

Kinachounganisha Mzanzibari wa uzawa wa Urabuni au Uhindini ni kukubali kuitwa MUAFRIKA, au siyo? Kinachounganisha Mhehe wa Iringa na Mhaya wa Bukoba na Muaha wa Kigoma ni kukubali kitwa MUAFRIKA, au siyo? Hivi ukianza kushabikia kuvunja nchi ya Tanzania iliyodumu zaidi ya miaka 49 (1964-2013) na kushabikia Utanganyika uliodumu miaka takribani 45 ( 1919-1964) (ambayo miaka zaidi ya 42 yake ilikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza na inawezekana Watanganyika wengi HAWAKUJITAMBUA kuwa walikuwa Watanganyika!) , una huhakika gani kuwa hii Tanganyika itakayo fufuliwa na wanasiasa wachovu wa kizazi hiki cha mafisadi waliojaa udini na ukabila haitamegeka pia vipande vipande kwa misingi ya ukabila na udini?
Kinachoweza kutuunganisha leo na jana hapa Tanzania ni kujitambuwa kuwa sisi ni WAAFRIKA, na UTANZANIA ni kituo cha kati kuelekea utambulisho ulio imara na wenye mashiko zaidi wa UAFRIKA MASHARIKI na UAFRIKA WA BARA ZIMA. Hayo ndiyo mawazo yangu na mimi si Napoleon au Bismark au Musolini, kwa hiyo niko tayari kukaa kwa huzuni kwa kukataliwa maoni yangu ninayodhani ni sahihi! NJE ya UZALENDO wa UMAJUMUI wa KIAFRIKA hakuna uzalendo mwingine zaidi ya ushabiki wa kibaguzi wa kidini na kikabila!!! I am an Afrikan! I am an East African! I am a Tanzania! I refuse to return to being a Tanganyikan after 49 years of liberation!!!
Mwl. Lwaitama

0 comments:

 
Top