Wagonjwa wa vidonda vya tumbo Nchini wanapaswa kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotolewa na madaktari wakati wote hasa katika matumizi ya vyakula vyenye Tindikali { Acid } ili kuondokana na maradhi hayo ambayo husababisha ukosefu wa utulivu wa kimaisha.

Kauli hiyo imetolewa na Mgunduzi wa Dawa ya asili inayotibu vidonda vya tumbo ijuilikanayo kwa jina la Fiterawa Dr. Rahabu Rubago wakati alipotembelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Bwawani Mjini Zanzibar.

Dr. Rahabu Rubago na Timu yake yupo Zanzibar tokea Tarehe 15 mwezi uliopita kufanya uchunguzi wa wagonjwa mbali mbali wa maradhi hayo sambamba na kutoa tiba pamoja na taaluma kwa wananchi wanaosumbuliwa na ugonjwa huo.

Mtaalamu huyo wa Tiba ya maradhi ya vidonda vya tumbo alivitaja baadhi ya vyakula muhimu vinavyowapa faraja wagonjwa wa maradhi hayo kuwa ni pamoja na chai ya soya, mchai chai, matunda pamoja na vyakula vya ngano.

Dr. Rahabu Rubago alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba maradhi ya vidonda vya tumbo yanaonekana kuendelea kukua siku hadi siku hapa nchini kufuatia msongamano wa maisha unaowakumba watu wengi katika maeneo mbali mbali.

Alisema katika kuisaidia jamii kuondokana na matatizo hayo Taasisi yake ya tiba ya maradhi ya vidonda vya tumbo {Rahabu Ulcers Clinic Centre } imejitolea kutoa taaluma kwa jamii kupitia vipindi maalum katika vyombo vya habari redio na Tv.

“ Tumekuwa tukiwapatia taaluma wananachi wetu katika sehemu mbali mbali kwa kutumia vyombo vya Habari. Lakini Vijijini tumejipangwa kuwapelekea pia Taaluma hiyo muhimu kwa kutumia vipeperushi “ . Alisisitiza Dr. Rahabu Rubago.

Dr. Rahabu amewahakikishia wananchi kwamba dawa ya Taasisi hiyo iko katika kiwango kinachokubalika Kitaalamu baada ya kufanyiwa utafiti na Kitengo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili na kuthibitishwa na mkemia Mkuu wa SMT na bodi ya vyakula, Dawa na vipodozi Zanzibar.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza cliniki hiyo ya tiba ya Vidonda vya Tumbo kutokana na juhudi za watendaji wake kujitolea kuisaidia Jamii Bara na Visiwani.

Balozi Seif alimuhakikishia Dr. Rahabu Rubago kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada utakaohitajika kwa uongozi wa Taasisi hiyo katika kuona mipango yake ya kusaidia Wananchi Kiafya pamoja na Taaluma inafanikiwa.

Dawa ya Fiterawa inayotibu vidonda vya tumbo ambayo imegunduliwa na Rahabu Ulcers Clinic Centre mnamo mwaka 1998 tayari imesha tibu na kuponya wagonjwa wasiopunguwa milioni moja ndani na nje ya Tanzania.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top