Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amewatahadharisha wakaazi wa Arusha kuilinda na kuitunza amani iliyopo ili kuuendeleza mji huo kiuchumi.

Amesema mji wa Arusha ni miongoni mwa miji muhimu katika maendeleo ya Tanzania kutokana na umaarufu wake na kuwa mji wa kitalii na biashara.

Maalim Seif ametoa tahadhari hiyo katika kata za Themi na Kaloleni mjini Arusha, wakati akiwahutubia wakaazi wa maeneo hayo kwenye mikutano ya kampeni za udiwani katika kata hizo.

Amefahamisha kuwa mji huo umeiletea sifa kubwa Tanzania na kupelekea kuwa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kituo muhimu cha mikutano ya kimataifa.

Ameongeza kuwa iwapo amani itatoweka katika eneo hilo, itaupotezea sifa mji huo na kushuka kwa mvuto wake wa kitalii, kibiashara na shughuli za kimataifa.

Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema wakaazi wa Arusha wana kila sababu ya kujivunia maendeleo na rasilimali zilizopo, yakiwemo madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Arusha pekee duniani kote.

Akizungumzia kuhusu kampeni, Maalim Seif amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu na kuvumiliana ili kutunza na kulinda amani iliyopo ambayo ni rasilimali kubwa kwa maendeleo ya nchi.

Amesema vyama vingi havikuja kwa lengo la kuwagawa au kuwafitinisha Watanzania, bali kutoa fursa kwa wananchi kuchagua chama au kiongozi wanayemtaka kwa uhuru.

Amewaomba viongozi wa vyama vya siasa kushindana kwa hoja na kuachana na tabia ya kuwalazimisha na kuwanyanyasa wananchi na kupelekea kuwakosesha haki na uhuru wao wa kuchagua na kuchaguliwa.

Wagombea udiwani kwa kata za Themi na Kaloleni kupitia Chama Cha CUF Lobora Petro Ndarpoi na Darwesh Abbass Ramadhan, kwa upande wao wamewaahidi wakaazi wa maeneo hao kuwatatulia kero zinazowakabili kwa muda mrefu zikiwemo upungufu wa ajira kwa vijana pamoja kuimarisha huduma za elimu mashuleni.

Wamesema maeneo hayo yana utajiri mkubwa wa viwanda lakini vingi kati ya hivyo havifanyi kazi vizuri, na hivyo kupoteza fursa za ajira kwa vijana, na kwamba iwapo watachaguliwa watashirikiana na halmashauri kuvifufua na kuviendeleza kwa maslahi ya wananchi wa Arusha.

Uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kata 26 nchini, unatarajiwa kufanyika tarehe 16/06/2013, baada ya madiwani waliochaguliwa katika kata hizo kupoteza sifa na wengine kufariki dunia.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top