Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameiagiza Wizara ya Kazi kusimamia utaratibu wa waajiri binafsi, ili kuhakikisha kuwa wanawapatia zote wafanyakazi wao ikiwa ni pamoja na malipo ya muda wa ziada.

Amesema serikali kwa upande wake imekuwa ikiendeleza utaratibu wa kuwapa malipo hayo wafanyakazi wake, lakini malalamiko mengi yamekuwa yakijitokeza kwa taasisi binafsi.

Maalim Seif ameeleza hayo viwanja vya Amaan mjini Zanzibar, wakati akifungua maonyesho ya nne ya biashara na huduma, ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani “Mei day”, yanayotarajiwa kufikia kilele chake kesho.

Kuhusu maonyesho hayo Maalim Seif amesema ni muhimu katika kujifunza mbinu za kibiashara na kubadilishana uzoefu kwa wajasiriamali.

Mapema akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kazi, Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haji Omar Kheir, amesema lengo la maonyesho hayo ni kukuza ajira kupitia vyama vya ushirika.

Katika risala yao ya maonyesho, wafanyakazi hao wamesema wanakabiliwa na tatizo la sehemu maalum ya kufanyia maonyesho, na kuiomba serikali kuwasaidia kupata sehemu hiyo.

Maonyesho hayo yamevishirikisha vikundi 48 vya wajasiriamali kutoka Unguja na Pemba.

Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top