Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Watanzania kuacha dhana ya kulihusisha tukio la mripuko unaodhaniwa kuwa ni bomu uliotokea katika Kanisa la Kikatoliki Wilayani Arumeru Mkaoni Arusha kuwa lisihushishwe na masuala ya Kidini wala Kisiasa.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kuangalia mareruhi wa mripuko huo waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha pamoja na kuwapa pole Viongozi pamoja na waumini wa Kanisa lililopata maafa hayo.

Balozi Seif alisema Tukio hilo ambalo linadalili zote za Kigaidi limeshitua Taifa na kuwakera Wananchi wote Tanzania Bara na Zanzibar na linafaa kulaniiwa na wapenda amani wote popote walipo.

Alifahamisha kwamba hiyo ni fitna inayojengwa katika kuleta chuki baina ya Serikali na Wananchi hasa waumini. Hivyo aliwanasihi Watanzania kuendelea kutulia na wala hakuna haja ya kuanza kutuhumiana ndani ya kipindi hichi kigumu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea fahaja yake kufuatia vyombo vya ulinzi kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wahusika wa mripuko huo wapatao 10 hadi hivi sasa ambao kati yao wane ni raia wa Saudi Arabia na Mmoja Raia wa Kenya.

Balozi Seif aliwahakikishia wananchi wote pamoja na waumini walioathirika na tukio hilo kwamba Serikali itahakikisha inawashikilia wale wote waliohusika na njama hizo na kuwachukulia hatua za kisheria kutokana na udhalimu wao huo.

“ Tungeliomba jambo hili baya lisitokezee tena katika Nchi yetu kwani linaonyesha kuleta fitna kati ya Serikali na Wananchi wake “ Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.

Akizungumzia suala la Kidini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali zote mbili zimetoa uhuru wa kuabudu ambao umo ndani ya katiba na kamwe haitavumilia kuona uhuru huo unaingiliwa na watu wachache.

Alisema matukio ya hujuma ndani ya majengo ya ibada yamekuwa yakiwapa hofu na wakati mgumu waumini kuendelea na ibada zao za kila siku.

“ Hofu hii iliyojengeka miongoni mwa waumini kutokana na hujuma wanazofanyiwa inawapa wakati mgumu wa kuabudu waumini hao “. Alifafanua Balozi Seif.

Akitoa shukrani kwa niaba yake na waumini wenzake Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Askofu Josephat Leburu alisema waumini wa jimbo hilo wamepata fafaja kubwa kufuatia ujio wa Viongozi mbali mbali wa Kitaifa waliofika kuwapa pole.

Askofu Josephat alisema moyo huu ulioonyeshwa na Vionmgozi wa Kitaifa umetoa sura sahihi uliyoonyesha ushirikiano wa karibu yao yao na WEananchi wanaowaongoza.

Hata hivyo Viongozi hao wa Kidini waliiomba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi kuendelea kutoa Taarifa kadri hatua zinavyochukuliwa za kukabiliana na tukio hilo waliloliita la kigaidi.

Walisema hatua hiyo itasaidia sana kupunguza joto la waumini wao ambalo wakati mwengine hufiki maamuzi ya kutaka kuchukuwa hatua mikononi mwao wakati wanapokabiliwa na matukio ya hujuma dhidi yao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nd. Nyerembe Munasa Sabi akitoa ufafanuzi wa baadhi ya changamoto za waumini hao alisema Serikali Kuu kupitia, Mkoa na Wilaya hiyo inaendelea na juhudi za kuwasaka wale wote waliohusika la mripuko huo.

Nd. Nyerembe alifahamisha kwamba hadi sasa watuhumiwa kumi wameshatiwa mbaroni kwa msaada wa wananchi wema ambapo kati yao wane ni raia wa Saudi Arabia na Mmoja Raia wa Kenya.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru alieleza kwamba tukio hilo la mripuko ni ishara ya ugaidi unaojenga chuki ambao umeandaliwa katika mazingira ya kitaalamu zaidi.

Aliwanasihi Viongozi na Waumini wa Kikristo Mkoani humo kuendelea kuwa wastahamilivu wakati Serikali kuu inajitahidi kujenga mazingira yatakayosaidia kuepusha mgawanyiko miongoni mwa Wananchi.

Ndugu Nyerembe Munasa Sabi pia alikemea tabia ya baadhi ya wana siasa kuanza propaganda ya kulinasbisha tukio hilo kuwa na uhusiano na Chama cha siasa.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru alieleza kuwa hadi sasa Mripuko huo ulisababisha vifo vya watu watatu, na wengine 66 kujeruhiwa ambapo mkapa muda huu watu 24 wamesharuhusiwa kurejea nyumbani na wengine 34 wanaendelea kupata huduma katika Hospitali ya Mkoa ya Arusha.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top