Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya Kibiashara ya Shanfar & Partners Co. L.L.C yenye Makao makuu yake Mjini Salala Nchini Omar imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyake hapa Zanzibar.

Nia hiyo imekuja kufuatia Visiwa vya Zanzibar kubarikiwa kuwa na rasilmali kadhaa ambazo bado hazijatumika katika kusaidia kuendeleza uchumi wa Taifa sambamba na kuongeza vipato kwa wananchi.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo Bwana Ali Omar Al–Sheikh akiuongoza ujumbe wa Viongozi watano wa Kampuni hiyo alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Ali Omar alisema ujumbe wake umeridhika na rasilmali kadhaa zilizomo ndani ya Visiwa vya Zanzibar baada ya kupata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali Mijini na Vijijini.

Alifahamisha kwamba Taasisi yao itaangalia maeneo inayoweza kuwekeza baada ya kufanya uchambuzi wa kina wakilenga zaidi katika Sekta ya Utalii ambayo Zanzibar tayari imeshafikia hatua kubwa katika kuimarisha miundo mbinu ya sekta hiyo.

“ Zanzibar tayari imeshafanikiwa vyema katika uwekezaji wa Hoteli za daraja linalokubalika Kimataifa. Kinachohitajika kwa wakati huu ni namna gani wanaweza kushajiisha makampuni ya kitalii kuweza kuitumia zaidi fursa hiyo “. Alifafanua Bwana Ali Omar.

“ Tumeliangalia hata zao la karafuu linalotegemewa kwa Uchumi wa Zanzibar ambalo pia linaweza kuimarishwa mauzo yake katika soko la Kimataifa kwa kutumiwa zaidi utaalamu wa kisasa “. Aliendelea Kusisitiza Mwakilishi huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Salala.

Naye Ofisa Mkuu wa Kampuni hiyo ya Shantar & Partners Bwana S. Srihar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba katika jitihada za kusaidia maendeleo ya Zanzibar Kampuni yao ina uwezo wa kuyashawishi mashirika na Makampuni ya Kimataifa ya watembezaji Watalii kulitumia soko la Zanzibar la Utalii katika kutembeza wateja na wageni wao.

Bwana Srihar alisema kufanikiwa kwa mpango huo kunaweza kutoa nafasi ya ajira kwa wazalendo waliowengi Nchini hasa lile kundi kubwa la vijana wanaomaliza masomo yao.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe huo wa Kampuni ya Shanfar & Partners ya Salala Nchini Oman kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea na juhudi za kuimarisha miundo mbinu katika sekta mbali mbali za Kiuchumi hapa Nchini.

Balozi Seif alifahamisha kwamba uimarishaji wa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Zanzibar ni miongoni mwa hatua hizo kwa lengo la kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Ujumbe huo wa Kampuni ya Kibiashara ya Shanfar & Partners kuitumia fursa hiyo ili isaidie uchumi wa Zanzibar sambamba na kuimarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Oman.

Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Shanfar & Patners Co. L.L.C ya Salala Nchini Oman imekuwa na ubia wa kibiashara na zaidi ya Makampuni saba ya Kimataifa katika Nyanja za Viwanda, Usafiri wa Anga, Utalii, huduma za Umeme, ujenzi na Uchapishaji.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top