Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa uwamuzi kwamba Mashamba yote ya Mikarafuu na Minazi ya Serikali yaliyokuwa chini ya Usimamizi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kuanzia sasa yatakuwa yakishughulikiwa na Wziara ya Kilimo na Mali Asili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa uamuzi huo wa Serikali wakati akizungumza na Masheha wote wa Mikoa Miwili ya Pemba hapo katika ukumbi wa Chuo cha Amali Vitongoji Chake Chake Pemba.

Balozi Seif alisema wakati suala la Ardhi litaendelea kubakia Wizara ya Ardhi amewaomba Masheha ambao maeneo yao yamo Mashamba ya Serikali ya Mikarafuu na Minazi na hadi sasa hayajahakikiwa watoe Taarifa kwa Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Pemba au Kiongozi yeyote atakayewekwa kwenye zoni.

Alisema udhibiti wa mapato yanayotokana na mazao yaliyomo kwenye baadhi ya mashamba ya Serikali yalikuwa yakileta mgongano kutokana na Mashamba hayo kushughulikiwa na Wizara mbili tofauti.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwapongeza Masheha wa shehia mbali mbali Kisiwani Pemba kwa juhudi zao za kusaidia uhakiki wa mashamba ya Serikali yaliyomo kwenye shehia zao.

Akizungumzia suala la udhibiti wa ukataji onyo wa Misitu Balozi Seif aliwakumbusha Masheha hao kuhakikisha kwamba wimbi la ukataji ovyo wa Miti unadhibitiwa.

“ Kijani ya Pemba tunataka ibakie kama kawaida na hili litafanikiwa iwapo wana jamii pamoja na masheha watashirikiana katika udhibiti wa ukataji ovyo wa misitu “. Alisisitiza Balozi Seif.

Wakielezea changamoto zinazowakabili baadhi ya Masheha hao walisema mazingira duni wakati wanapostaafu utumishi wao pamoja na mfumko wa hujuma wanazofanyiwa masheha limekuwa tatizo kubwa linalopunguza ari ya utekelezaji wa majukumu yao.

Masheha hao waliiomba Serikali Kuu kujenga mazingira yatakayowawezesha kupatiwa mikopo ya vyombo vya usafiri ili kurahisisha kazi zao masuala ambayo Balozi Seif aliahidi kwamba Serikali itayazingatia na kuyapatia ufumbuzi unaofaa.

“ Ninazichukuwa changamoto zenu zote zinazowakabili ambazo ni za msingi kabisa na sisi kama Serikali tutazizingatia na kuona namna gani tunazipatia ufumbuzi unaofaa. Tunaelewa kwamba nyinyi masheha ni sehemu ya Serikali “. Balozi Seif alikuwa akijibu baadhi ya changamoto za masheha hao.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikagua shamba la Mikarafuu liliopo Kijiji cha Kinyasini Mtambwe la Ekari Tisa lambalo lilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi na kupongeza hatua iliyofikiwa ya usafishaji wa shamba hilo lililokuwa katika hali mbaya.

Pia aliangalia shamba la Mikarafuu la Daya Mtambwe linalomilikiwa na Wizara ya Kilimo lenye Ekari zaidi ya 37 ambalo limeathirika kutokana na maendeleo ya ujenzi wa Bara bara ambapo jumla ya miti 290 ya mikarafuu ililazimika kukatwa kutokana na ujenzi huo.

Baadaye Balozi Seif alikagua shamba la Minazi la Tumbe ambapo Uongozi wa Wizara ya Ardhi unalikabidhi shamba hilo la ekari 45 kwa Wizara ya Kilimo kwa vile liko katika eneo la Ukanda wa Utafiti wa Kilimo.

Afisa Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali asili zisizorejesheka Pemba Nd. Said Juma Ali alimueleza Balozi Seif kwamba Ekari kumi tayari zimeshaoteshwa minazi mipya ya asili { East Africa }.

Nd. Ali alisema kituo cha Utafiti wa Kilimo Pemba kinaendelea na harakati za kurejesha minazi ya asili kwa kuotesha mbegu zitakazouzwa kwa wakulima katika maeneo mbali mbali ili kuziba pengo la minazi mipya ambayo uzalishaji wake huchukuwa kipindi kifupi.

Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisisitiza kwamba zao la nazi bado linabaki kuwa na tija katika pato la taifa na mkulima binafsi.

Balozi Seif aliwagiza watendaji wa Sekta ya Kilimo kupanga utaratibu maalum utakaowasaidia wakulima Taaluma itakayowapa njia na fursa ya kuendeleza kilimo hicho kwa ufanisi mkubwa.

“ Mnazi ni miongoni mwa mti uliobarikiwa kuwa na sifa na vitu vyake kutumika katika mambo mbali mbali tukitolea mfano Kifuu, usumba, makosi, nazi, makuti, madafu pamoja na kigogo chake kwa ajili ya utengenezaji wa mapambo ya samani “. Alifafanua Balozi Seif.

Naye kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Ndugu Hemed Salum alisema Mashamba mengi ya Mikarafuu na Minazi ambayo yalikuwa chini ya Usimamizi wa Wizara hiyo ni yale ambayo waliopewa na Serikali wamefariki dunia au kuhama Nchini.

Ndugu Hemedi alifahamisha kwamba mashamba hayo ni miongoni mwa zile eka tatu tatu zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top