Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Awena Sinani Massoud, amesema kazi ni kigezo muhimu cha kulinda heshma ya mwanamke.
 
Mama Awena ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya kutembelea jumuia ya maendelo ya wanawake wa Tundauwa (JUMWATU), ambao wanajishughulisha na kilimo cha mpunga, mihogo, migomba, ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira.

Amewapongeza akinamama hao kwa kuamua kujishughulisha na kujiongezea kipato, badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini.

Amewataka kujiongezea elimu katika sekta ambazo wameamua kuzifanyia kazi, ili waweze kufanya shughuli hizo kwa uhakika.

Aidha Mama Awena amewashauri akinamama hao kuwatumia wataalamu wa kilimo katika kupata ushauri wa kitaalamu kwa upande wa kilimo na muongozo mzuri wa ufugaji wa nyuki.

Kuhusu mazingira mama Awena amesema dunia nzima sasa imefadhaishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi hali inaochangiwa na ukosefu wa kutojali mazingira.

Amewatahadharisha akinamama hao wakati wakifanya shughuli hizo wahakikishe wanazingatia athari za kimazingira na kuyawacha yakiwa salama dhidi ya uharibifu wa aina yoyote.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Mwanajuma Majid Abdalla amesema kinamama wanakabiliwa na changamoto kubwa ya muonekano wa kuwa ni watu wanaostahiki kukaa na kufanya shughuli za nyumbani. 
 
Hivvo kujitokeza kwao kuunda jumuiya na kuweza kujiajiri wenyewe ni hatua kubwa ya kimaendeleo kwa wanawake hao sambamba na kuepukana na utegemezi.

Na Mauwa Mohd- Pemba.

0 comments:

 
Top