Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wananchi kushirikiana kuisaka misumeno ya moto popote ilipo ili iweze kutokomezwa kabisa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Ameeleza hayo katika kampeni maalum ya kutokomeza misumeno ya moto ambapo misumeno 23 imechomwa moto mbele ya kiongozi huyo, baada ya kukamatwa na maofisa wa Idara ya misitu.

Amesema kila mtu ana wajibu wa kushirikiana na jamii katika kufichua misumeno iliyobakia, ili kuhakikisha kuwa haitumiki tena na kusababisha athari za kimazingira.

“Kila mtu ana wajibu wa kuwafichua watumiaji wa misumeno hii, lakini mashena na polisi jamii muna jukumu kubwa zaidi, na nina hakika mukiamua munaweza kuwabaini wote wenye misumeno ya moto”, alisema Maalim Seif.

Amesema iwapo misumeno hiyo haitodhibitiwa inaweza kuiathiri nchi kwa kiasi kikubwa kutokana na uwezo wake wa kukata miti kwa muda mfupi.

Uchomaji huo wa misumeno ya moto 23 umefanyika katika ofisi za Idara ya misitu iliyoko Kizimbani Kisiwani Pemba.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya kilimo na maliasili Affan Othman Maalim amesema misumeno ya moto ipatayo 270 bado inakisiwa kuwepo Zanzibar, na kwamba kampeni hiyo itasaidia kuitokomeza.

Kwa mujibu wa Affan, kisiwa cha Pemba kinaongoza kwa kuwa na misumeno mingi ya aina hiyo ipatayo 150, huku Unguja kukiwa na misumeno zaidi ya 120.

Amefahamisha kuwa takriban ekari 1000 za miti hupotea kila mwaka visiwani Zanzibar kutokana na kukatwa ovyo na kuongezeka kwa kasi hiyo kutokana na matumizi ya misumeno ya moto.

Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili Mtumwa Kheir Mbarak, amesema misumeno hiyo ambayo ni adui wa muda mrefu wa mazingira, inaweza kuiweza kuifanya nchi kuwa jangwa kwa muda mfupi na ni hatari pia kwa afya ya binadamu.

Maalim Seif yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambako anatembelea shughuli za kilimo kwa lengo la kuwahamasisha wakulima kuendeleza kilimo chenye tija kwa kutumia utaalamu wa kisasa na mbegu bora.

Katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambako alianza ziara yake alitembelea shamba la utafiti wa uzalishaji wa mpunga wa mbegu ya nerika liloko Gombeume mchangamdogo, skuli ya wakulima iliyoko Kiongweni Kambini, shamba la viazi vitamu Makangale na skuli ya wakulima juu ya nishati mbadala iliyoko Kinyasini.



Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top