Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amesema Wananchi wa Jimbo la Chambani Mkoa Kusini Pemba wanapaswa kujenga Historia mpya ya kumsimamia kushinda Kijana wa CCM atakayeungana nao katika kujiletea Maendedleo yao kwa haraka.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizindua Mkutano wa Kampeni za CCM kuelekea kwenye uchaguzi mdogo wa Kiti cha Ubunge wa Jimbo la Chambani hapo katika uwanja wa Michezo wa Skuli ya Ukutini Wilaya ya Mkoani.
Uchaguzi huo unakuja kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Salim Hemed Khamis kufariki Dunia kutokana na Maradhi ya Moyo mnamo Tarehe 26 mwezi wa machi mwaka huu wa 2013.

Balozi Seif ambae pia alipata fursa ya kumnadi Mgombea wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Mattar Sarhan Said kwenye Mkutano huo wa uzinduzi ya Kampeni alisema wakati wa kujipima mawazo yao na yale wanayopewa na kuletewa umefika ili watoe maamuzi sahihi yatakayoleta maslahi kwao na vizazi vijavyo.

Alieleza kwamba Wananchi wa Jimbo la Chambani wamekuwa mashahidi wakubwa wa kuona Ilani za Vyama vya siasa zinaponadiwa wakati wa kampeni za uchaguzi tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwakumbusha wanachi hao kwamba CCM iliyopata ridhaa ya kuongoza Dola Bara na Zanzibar imekuwa ikiendelea kutekeleza ilani yake kama ilivyoahidi ambapo Jimbo la Chambani limefarajika na Ilani hiyo hasa katika sekta ya Elimu, Afya na Mawasiliano.

Akizungumzia amani Balozi Seif alisema kwa vile suala hilo limo ndani ya Ilani ya uchaguzi ya CCM Serikali zote mbili zitaendelea kuwa imara katika kuhakikisha zinadhibiti amani iliyopo hivi sasa.

Alisema vipo baadhi ya vikundi na watu wanaojaribu kuichezea amani iliyopo kwa visingizio vya uhuru wa kusema ambavyo kamwe Serikali haitakuwa na mzaha katika kukabiliana navyo.

“ Katika suala la amani tuko wazi kabisa, hatutamvumilia Mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuhatarisha amani ya Nchi. Lazima Jamii ichunge amani ya Nchi iliyopo “. Alitahadharisha Balozi Seif.

Kuhusu suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif alisema kwamba Wazanzibari ndio wanaoendelea kufaidika zaidi Muungano uliopo ambao uliasisiwa na Hayati Mwalimu Julius K.Nyerere pamoja na Mzee Abeid Amani Karume.

Alisema huduma za Kiuchumi na biashara zimepanuka na kushamiri zaidi kwa pande zote mbili ikilinganishwa na wakati wa kabla ya Uhuru hali iliyowafanya Wazanzibari walio wengi kuendelea Kibiashara.

Aliwatahadharisha Wananachi kujiepusha na kasumba wanayoendelea kupewa kuhusu mfumo wa Muungano unaotakiwa na kuwashauri kuiachia Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kufanya kazi hizo kwa niaba yao.
Katika Risala yao iliyosomwa na Katibu Msaidizi Mkuu wa CCM Wilaya ya Mkoani Nd. Abdulla Yussuf wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Chambani wameelezea kujivunia kwao kwa kuendelea na shughuli zao za kimaisha bila ya hofu wala vikwazo.

Nd. Abdulla alisema Wananchi hao wameahidi kuilinda kwa nguvu zote amani iliyopo Nchini na kusisitiza kwamba wakati wa kusikiliza na kuunga mkono propaganda za watu binafsi umekwisha na wameamua kuzipa kisogo.

Walifahamisha kwamba Chama cha Mapinduzi ni nahodha wa Demokrasia kwa kuleta mambo mengi ya maendeleo ambayo yameenea na kuchanua kila pembe ya Nchi hii likiwemo Jimbo la Chambani.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua Mkutano huo wa Kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chambani kwa Kiti cha Ubunge alisema CCM imedhamiria kushinda katika uchaguzi huo.
Nd. Vuai aliwaomba Wananchi wa vijiji vilivyomo ndani ya Jimbo hilo wanawake, wazee na Vijana kumuunga mkono mgombea wa CCM ili apate fursa ya kusimamia vyema Ilani ya Chama hicho katika Jimbo hilo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top