Matumaini ya Wananachi katika kupokea na hatimae kuangalia matangazo ya Televisheni kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } yatarejea endapo watendaji wa Shirika hilo kwa kushirikiana na Viongozi wao watajipanga vyema katika kutekeleza majukumu yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya ghafla katika Kituo cha Televisheni cha Shirika hilo kilichopo Karume House kuangalia matatizo yaliyopelekea kukosekana kwa matangazo ya Habari Kituoni hapo.

Akizungumza na Uongozi wa Shirika hilo na baadae Watendaji wake Balozi Seif alisema Serikali iliamua kuunda Shirika hilo lengo likiwa ni kuimarisha zaidi matangazo yake pamoja na kwenda sambamba na mabadiliko ya mfumo wa utendaji katika sekta ya Habari Duniani.

Balozi Seif alisisitiza kwamba wakati umefika hivi sasa kwa Shirika hilo kuendeshwa kibiashara, na hilo litafikiwa iwapo Taasisi zinazoendelea na zile zinazotumia na kuhitaji huduma za matangazo za Shirika hilo zitalipa.

“ Sisi Serikalini tumeshaliagiza Baraza la Wawakilishi ambalo liko chini ya Wizara yangu lianze kulipa fedha wakati linapoendelea na vikao vya Baraza katika matangazo yake ya moja kwa moja. Dodoma Shirika la Utangazaji Tanzania TBC wanalipwa na Bunge wakati wanaporusha matangazo yao utaratibu ambao hata sisi wabunge tunachangia suala hilo “. Alifafanua Balozi Seif.

“ Katika kujenga mahusiano mema baina ya Taasisi hizo inaweza kuruhusiwa kutangazwa bure wakati wa kipindi cha maswali na majibu “. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akizungumzia suala la uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaonya watendaji hao kuwepuka tabia ya fitna baina yao na Viongozi jambo ambalo linarejesha nyuma ufanisi wa kazi zao.

Alikemea kwamba Kiongozi ye yote ambae atapenda kutanguliza fitna na majungu mbele aelewe kwamba anajiingiza katika mfumo mbaya wa kazi unaosababisha kuyeyusha haki za wafanyakazi wake.

Hata hivyo Balozi Seif aliwapongeza Watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } kwa utendaji wao wa kizalengo licha ya kukabiliwa na mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yao waliyopangiwa.

Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar alisema Vituo vya Matangazo ya Televisheni haviwezi kufanya kazi zake kwa mpangilio wa bajeti kama zinavyofanya Idara nyengine.

Alisema Uongozi wa Shirika hilo umekuwa akitoa Taarifa za maandishi wakati yanapotokea matatizo hasa suala kubwa la vifaa na uharibikaji wa mashine lakini ufumbuzi wake huchukuwa muda mrefu kutokana na mfumo wa matumizi uliopo.

“ Tumekuwa tukiiandikia Wizara kuijuilisha matatizo yetu yanapotokea lakini hatua zinazochukuliwa za kusubiri fedha hupelekea hata vile vifaa vya dharura vikaharibika baada ya kukosa usaidizi wa ziada “. Alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa ZBC Nd. Chande.

Hata hivyo Ndugu Chande alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Shirika hilo tayari umeshachukuwa hatua za dharura kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwasiliana na makampuni yanayotengeneza vifaa vinavyohitajika kituoni hapo kwa wakati huu wa dharura.

Alisema lengo la Shirika hilo katika mpango wake wa kuingia katika matangazo ya Kisasa ya Digital ni kuwa na mashine 10 za kurikodia vipindi zitakazotosheleza kabisa mahitaji ya vitengo vya Habari, Vipindi pamoja na Matangazo.

Kwa upande wao watendaji wa shirika hilo la Utangazaji Zanzibar wameelezea changamoto wanazopambana nazo kituoni hapo ambazo zimekuwa zikirejesha nyuma hamu na utendaji wao wa kazi za kila siku.

Walizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu usafiri wa uhakika wa kufuatilia Vipindi, Habari na hata kurejeshwa majumbani wakati wa usiku, ukosefu wa Bajeti za Vipindi, uchakavu wa Mashine za Matangazo, Haki za Wafanyakazi kama maposho na fedha za likizo pamoja na majungu na fitina baina ya Viongozi na Wafanyakazi.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top