Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imemuagiza mwekezaji aliyepewa eneo la Magofu ya Kihistoria liliopo Bweleo Wilaya ya Magharibi kuhakikisha kwamba ameshakamilisha shughuli zake za uwekezaji na kuanza kutoka huduma kama alivyoahidi katika mkataba wake ndani ya kipindi cha Mwaka mmoja kuanzia leo.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Mwekezaji huyo Bwana Chandra, Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya watu wa Bweleo, Sheha wa Shehia ya Bweleo, Mkurugenzi Zipa pamoja na Mkurugenzi Mazingira hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema ameridhika na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Maalum aliyoiteua kuchunguza mgogoro wa eneo hilo Tarahere 28 Oktoba mwaka 20112 kati ya Mwekezaji huyo na wananachi wa Bweleo waliyoiomba Serikali Kuu kumnyang’anya eneo hilo Mwekezaji huyo baada ya kukaa nalo kwa miaka mingi bila ya faida ya Wananchi hao.

Akifafanua baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo Maalum ya kuchunguza mgogoro wa eneo hilo ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi Mh. Abdulla Mwinyi, Balozi Seif alimtaka Mwekezaji huyo kuhakikisha kwamba mradi wake unafaidisha kimapato Wananchi wa maeneo hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema njia pekee ya kuepuka migogoro ndani ya sekta ya uwekezaji ni kwa wananchi wenyewe kuiachia Serikali kuu kutimiza waji wake kwa kutiliana saini ya mikataba na wawekezaji ili kuwepuka ujanja unaopelekea kuleta mzozo hapo baadaye.

“ Moja kati ya suala nililolishuhudia wakati wa ziara yangu mwaja jana katika eneo hilo ni lile lalamiko la wananchi hao la kuzibiwa njia wanayoitumia wakati wanapotoka katika shughuli zao za uvuvi. Hili unapaswa kulichukulia hatua mara moja kwa kushirikiana na Uongozi wa Shehia, Zipa na Mazingira “. Balozi Seif alimuagiza Mwekezaji huyo.

Hata Hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwekezaji huyo Bwana Chandra kwa hatua yake ya kusaidia maendeleo ya Wananachi wa Vijiji vinavyouzunguuka mradi huo na kumuomba asichoke kuendelea kufanya hivyo ili kujenga uhusiano mwema na Wananchi hao.

Balozi Seif aliusisitiza Uongozi wa mradi huo kuwasiliana na Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA }, Mipango Miji pamoja na Idara ya Mazingira ili kuhakikisha kwamba mradi huo unaendeshwa katika misingi iliyokubalika kutekelezwa Kisheria.

Eneo la Magufu ya Kihistoria la Bweleo limekuwa na mzozo wa muda mrefu kati ya Mwekezaji wake Bwana Chandra na Wananchi wa Vijiji vilivyolizunguuka eneo hilo wakidai Mwekezaji huyo kushindwa kuliendeleza kama ilivyokubalika.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top