Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Mhe. Fatma Ferej hakupendelewa kupewa tunzo ya mwanamke jasiri Tanzania kwa mwaka 2013 bali amestahiki kutokana na utendaji wake.

Akizungumza katika hafla maalum ya kumpongeza Mhe. Fatma Fereji kutokana na kupewa tunzo hiyo na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania tarehe 4/3/2013, Maalim Seif amesema Fatma Ferej ni mchapa kazi wa kweli na jasiri katika kutekeleza majukumu yake.

Amesema akiwa msaidizi wake katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais , Fatma Ferej amekuwa akimsaidia kwa karibu hasa katika kufuatilia masuala ya dawa za kulevya, mazingira na maendeleo ya watu wenye ulemavu.

Pia alimsifu kutokana na busara na mashirikiano yake na watendaji wengine wa Ofisi hiyo. “Sijawahi kupokea malalamiko kuwa Mhe. Fatma anawanyanyasa wafanyakazi wake, bali siku zote namuona ni kiongozi mwenye busara na mashirikiano makubwa”, alifahamisha Maalim Seif.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema Tunzo aliyoipata Fatma Ferej imekijengea sifa kubwa chama chake cha CUF.

Prof. Lipumba alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kutowabagua watoto wao na kuwapa fursa sawa za kielimu ili waweze kujiandaa vyema kukabiliana na maisha, sambamba na kuwapa fursa wanawake waweze kushiriki shughuli za kijamii.

Nae Mhe. Fatma Ferej amesema anaichukulia tunzo hiyo kama ni changamoto ya kuzidi ari ya kiutendaji, na kuwataka wanawake wajiamini wanapotekeleza majukumu yao.

Amefahamisha kuwa wakati umefika kwa wanawake kuuthibitishia ulimwengu kuwa wanaweza, na kuondokana na mtazamo finyu kuwa kazi za wanawake ni kukaa jikoni pekee.

Hafla hiyo ya pongezi maalum iliyofanyika hoteli ya Bwawani, iliandaliwa na Jumuiya ya wanawake wa CUF.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top